MAAFISA MAENDELEO YA JAMII NA WANANCHI KAHAMA WAUNGANA KUFANYA USAFI KUJIANDAA NA MVUA ZA EL NIÑO


Na Mwandishi wetu

Timu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wa Kata za Mhongolo na Majengo, leo Septemba 22, 2026, imeshiriki zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya kata hizo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea msimu wa mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni.

Zoezi hilo limewalenga wananchi katika kuhamasisha umuhimu wa kutunza mazingira, hususan kuondoa taka, kusafisha maeneo ya makazi na biashara pamoja na kuhakikisha mifereji na maeneo mengine ya kupitisha maji yanakuwa katika hali nzuri, ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.


Akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Bw. Elia Moshi, amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na kwamba, usafi ni hatua muhimu katika kuzuia magonjwa yakiwemo ya mlipuko, pamoja na changamoto nyingine zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.

Amesema mazingira machafu yanaweza kuchangia kuzaliana kwa mbu waenezao Malaria na vimelea vya magonjwa  ya mlipuko kama Kipindupindu, huku taka zinazoziba mifereji zikiongeza hatari ya maji kusimama na kukosa uelekeo hali ambayo inaweza kusababisha mafuriko.


“Naomba sisi sote tuwe wazalendo wa kutunza mazingira yetu. Tunaelekea kipindi ambacho mvua za awali zinatarajiwa kunyesha kwa wingi. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetutangazia uwepo wa El Niño, hivyo ni muhimu tujiandae,” amesema Bw. Moshi.

Amewataka wananchi kutotupa taka kwenye mifereji na maeneo ya wazi, huku akiwaomba kuwa mabalozi wa usafi katika familia, maeneo ya makazi na biashara ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote.


Aidha, amewasisitiza kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa taarifa kuhusu maeneo yenye taka nyingi, maji yaliyotuama, mifereji iliyoziba pamoja na maeneo mengine yanayoweza kuhatarisha afya na usalama wa jamii wakati wa msimu wa mvua.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi hilo, wamesema usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na kwamba, ushiriki wao katika kufanya usafi ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.

Wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi, huku wakitoa wito kwa wananchi wengine kuacha tabia ya kutupa taka ovyo na badala yake wazikusanye kwa ajili ya kwenda kutupwa kwenye maeneo yalitengwa kwa ajili ya taka.


Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi wa mazingira na kuchukua tahadhari mapema, ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza mvua za El Niño ziakapoanza kunyesha

Post a Comment

0 Comments