MIGOGORO YA KIMAHUSIANO NA WIVU WA KIMAPENZI, ZIMWI LINALOKATISHA UHAI WA WENGI

Watu 1,605 wameuawa nchini kutokana na migogoro ya kimahusiano katika kipindi cha mwaka 2024 hadi Juni 2026, huku wanawake na watoto wakitajwa kuwa miongoni mwa waathirika wa matukio hayo, kwa mujibu wa waraka wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Waraka huo uliotolewa Oktoba 22, 2026, unaeleza kuwa takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha matukio 941 ya mauaji yaliripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026, ikilinganishwa na 926 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
Kati ya matukio hayo 941 yaliyoripotiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, 458 yalihusishwa na migogoro ya kimahusiano.
Waraka huo unaeleza kuwa mwaka 2024 yaliripotiwa matukio 2,193 ya mauaji, ambapo 422 yalihusishwa na migogoro ya kimahusiano. Mwaka 2025, matukio ya mauaji yalifikia 1,977, yakiwamo 725 yaliyohusishwa na migogoro hiyo.
THRDC imesema migogoro hiyo inahusishwa na sababu mbalimbali, zikiwamo wivu wa kimapenzi, migogoro ya ndoa na familia, madai ya usaliti, tofauti za kifedha na changamoto za malezi ya watoto.
Katika waraka huo, mtandao umetaja matukio mbalimbali ya mauaji yaliyoripotiwa kati ya Julai na Oktoba 2026, yakiwamo ya Leah Mazengo wa Bahi, Dodoma, na Margeth Hamis Richard wa Musoma, mkoani Mara.
Pia, umeeleza kuhusu watoto wawili, msichana wa miaka minane na mvulana wa miaka 10, waliouawa na baba yao mkoani Morogoro kabla ya mwanaume huyo kujiua.
Kwa mujibu wa THRDC, baadhi ya matukio ya mauaji hutokea baada ya viashiria vya ukatili kujitokeza kwa muda mrefu, vikiwamo vitisho vya kuua, vipigo vya mara kwa mara, kumdhibiti mwenza na unyanyasaji wa kisaikolojia.
Mtandao huo umetaja pia udhaifu wa mifumo ya kuzuia ukatili, ukosefu wa elimu kuhusu mahusiano salama, changamoto za afya ya akili na upungufu wa wataalamu wa ustawi wa jamii na huduma za ushauri nasaha kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.
Kutokana na hali hiyo, THRDC imeitaka Serikali kuimarisha mifumo ya kupokea na kufuatilia taarifa za vitisho, kuongeza Maafisa Ustawi wa Jamii na kuweka mifumo madhubuti ya kuwalinda watu walio katika hatari ya kufanyiwa ukatili.
Pia, mtandao huo umelitaka Bunge kutunga sheria mahsusi ya kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani. Umeziomba taasisi za elimu, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii kuimarisha elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.
Katika hatua nyingine, THRDC na mashirika mengine ya utetezi wa haki za binadamu yametangaza kampeni endelevu yenye kaulimbiu “Mapenzi Siyo Vita; USIUE”, inayolenga kuhamasisha jamii kukataa ukatili na kuheshimu haki ya kila mtu kuishi na kufanya maamuzi kuhusu mahusiano yake.
Mtandao huo umesisitiza kuwa migogoro ya kimapenzi haiwezi kuhalalisha mauaji, na kwamba mahusiano yanaposhindikana, wahusika wanapaswa kutafuta suluhisho la amani au kuachana bila kutumia vitendo vya ukatili.

SOURCE-IPP MEDIA

Post a Comment

0 Comments