WAZIRI KAPINGA KESHO KUFUNGUA RASMI MAONESHO YA 5 YA KITAIFA YA SIDO KATIKA MANISPAA YA KAHAMA

 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb)

Na George Mganga, Kahama MC


Maonesho ya Kitaifa ya Shirika la Maendeleo ya viwanda vidogo (SIDO) yameanza rasmi Oktoba 21, 2026, katika Uwanja wa Magufuli uliopo Kata ya Majengo, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, yakilenga kuwakutanisha wajasiriamali, wazalishaji na wadau wa sekta ya viwanda vidogo kwa ajili ya kuonesha bidhaa, huduma na fursa mbalimbali za kibiashara.

Hadi sasa, zaidi ya washiriki 200 wamesajiliwa na kuthibitishwa kushiriki katika maonesho hayo, huku zoezi la usajili likiendelea kwa washiriki wengine wanaotarajia kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa zao na kukuza biashara zao.

Ufunguzi rasmi wa maonesho hayo unatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi, Oktoba 24, 2026, ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Maonesho hayo yataendelea hadi Oktoba 30, 2026, yakitoa fursa kwa wajasiriamali wadogo na wazalishaji kukutana na wateja, kubadilishana uzoefu, kutangaza bidhaa zao na kujenga mahusiano ya kibiashara yanayoweza kusaidia kukuza shughuli zao za uzalishaji.

Aidha, maonesho hayo ni fursa kwa wananchi kutembelea viwanja hivyo, kujionea bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali, pamoja na kutambua ubunifu na mchango wa sekta ya viwanda vidogo katika kukuza uchumi na kujenga ajira.

Wananchi, wajasiriamali na wadau mbalimbali wanaalikwa kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Magufuli, Kahama, kushiriki na kunufaika na fursa zinazotolewa kupitia maonesho hayo.

Kaulimbiu ya manesho hayo kwa mwaka huu 2026 inasema kuwa "Teknolojia na soko, chachu wa viwanda vidogo nchini"

Post a Comment

0 Comments