Hafla hiyo, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ngazi ya wilaya na mkoa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Mhita, amempongeza Dk. Mlacha kwa kuaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, huku akimtaka kwenda wilayani humo na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Nakupongeza sana kwa kuteuliwa na Rais wetu kuwa Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama. Karibu Shinyanga kwenye timu ya ushindi,” amesema Mhita.
Aidha, Mhita amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato, kubuni na kuibua vyanzo vipya vya mapato, pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za halmashauri.
Amezitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu na michango ya wananchi, pamoja na kulipa madeni ya wazabuni ili kuepuka kuzalisha madeni mapya.
Wakati huohuo, Mhita emewaagiza viongozi wote wa wilaya wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri kuweka utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mhita pia amesisitiza umuhimu wa kusimamia usafi wa mazingira, ikiwamo kuzibua mitaro na kuchukua hatua za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Kwa upande wake, Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama, Dkt.Francis Daudi Mlacha, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuiongoza Wilaya ya Kahama.
Dkt. Mlacha ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza maagizo yote aliyoyapokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, akisema moja ya mambo atakayoanza nayo ni kushughulikia changamoto ya miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo.
Amesema pia atahakikisha kuna ongezeko la kasi katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za maendeleo.
Dkt. Mlacha ameteuliwa kuwa mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama siku chache zilizopita, baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kufanya uteuzi na uhamisho wa wakuu wa wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri.




























0 Comments