Padre Masolwa ametoa wito huo wakati akiadhimisha Misa ya Sherehe ya Somo wa Jumuiya ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Parokia ya Ndala, ambapo amemtumia Mtakatifu Papa Yohane Paulo II kama mfano wa kuigwa katika kusamehe, hata pale mtu anapokabiliwa na maumivu makubwa kutokana na makosa ya wengine.
| Padre Simon Masolwa |
Amesema
binadamu wote wana mapungufu na wanaweza kukoseana, lakini uwezo wa kusamehe na
kuomba msamaha ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kuponya majeraha ya
kihisia, kuondoa chuki na kuzuia visasi vinavyoharibu mahusiano katika jamii.
Akifafanua mfano wa Mtakatifu Papa Yohane Paulo II, Padre Masolwa amekumbusha tukio la Mei 13, 1981, ambapo kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alipigwa risasi na kujeruhiwa na Mehmet Ali Ağca, raia wa Uturuki, katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican.
![]() |
| Mtakatifu Papa Yohane Paulo II |
![]() |
| Papa Yohane Paulo II alipomtembelea Ağca gerezani Desemba 27, 1983 |
Padre
Masolwa amesema mfano huo unapaswa kuwafundisha watu kuwa kusamehe si ishara ya
udhaifu, bali ni uamuzi unaoweza kumkomboa mtu kutokana na mzigo wa chuki,
hasira na maumivu ya kihisia.
Ameonya kuwa
kutosamehe kunaweza kuendeleza migogoro ya kifamilia na kijamii, ikiwamo baina
ya wanandoa, ambao wakati mwingine hushindwa kuishi kwa upendo, kusaidiana na
kutimiza wajibu wao kutokana na makosa ya zamani ambayo hawajayamaliza kwa njia
ya mazungumzo na msamaha.
Amewahimiza
wanandoa kuachana na kiburi, kuwa tayari kuzungumza wanapokoseana na kujenga
moyo wa kusameheana ili kulinda amani ya familia na kuhakikisha watoto
wanakulia katika mazingira yenye upendo na mshikamano.
Aidha, amewataka watu wanaowakosea wengine kutambua maumivu wanayosababisha, kuomba msamaha kwa dhati na kujitahidi kutorudia makosa hayo.
Kwa upande mwingine,
amewahimiza waliokosewa kuwa tayari kusamehe na kujenga upya mahusiano yao.
Amesisitiza
kuwa msamaha haupaswi kuwa kisingizio cha kuendeleza makosa au ukatili, bali
uambatane na kutambua kosa, kuwajibika na kuchukua hatua zinazosaidia kuzuia
madhara kujirudia.
Wakati huohuo,
Padre Masolwa amezindua rasmi Jumuiya ya Mtakatifu Yohane Paulo II,
iliyoanzishwa Machi 1, 2026, baada ya kumegwa kutoka sehemu ya Jumuiya ya
Mtakatifu Maria Magdalena.
Misa hiyo
pia ilihudhuriwa na wawakilishi wa madhehebu mbalimbali ya dini, wakiwamo
Waislamu, Waadventista wa Sabato na wawakilishi wa makanisa ya Kipentekoste,
pamoja na viongozi wa kijamii akiwamo mwenyekiti wa mtaa.
Ushiriki wa
wawakilishi hao umeonyesha umuhimu wa kuvuka mipaka ya tofauti za kidini na
kijamii katika kujenga umoja, kuheshimiana na kuimarisha upendo miongoni mwa
watu.
Ujumbe wa
Padre Masolwa unaikumbusha jamii kuwa amani huanzia katika mahusiano ya kila
siku, kutambua makosa, kuomba msamaha na kuwa tayari kusamehe. Hatua hizo
zinaweza kusaidia kuvunja mzunguko wa chuki na visasi, na kujenga familia na
jamii yenye mshikamano.



0 Comments