KIUT KUTOA UFADHILI WA HADI ASILIMIA 50 KUWAWEZESHA WENYE KIPATO CHA CHINI KUPATA ELIMU YA JUU

Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania, Kampala International University in Tanzania (KIUT), kimeeleza dhamira yake ya kuhakikisha wanafunzi na watu wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya kati na ya juu kwa kutoa ufadhili (Scholarship) wa ada ya masomo wa hadi asilimia 50 kwa baadhi ya kozi muhimu.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutambulisha huduma za chuo hicho katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Shinyanga, Afisa Masoko wa KIUT, Gaudence Tracy, alisema chuo hicho kinaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa kuanzia ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili hadi Shahada ya Uzamivu (PhD), pamoja na fursa za ufadhili zinazopatikana.

Alisema ufadhili huo unalenga zaidi kozi za Sayansi ya Jamii, ambapo wanafunzi wanaweza kupata punguzo la ada hadi asilimia 50 kulingana na sifa na masharti yaliyowekwa. Aidha, kwa wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu kutoka serikalini isiyofikia asilimia 100 ya mahitaji yao, KIUT itasaidia kugharamia sehemu ya gharama inayobaki ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao bila vikwazo vya kifedha.

Afisa Masoko wa KIUT, Gaudence Tracy

“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba kila mtu mwenye sifa za kujiunga na elimu ya juu anapata nafasi hiyo bila kuzuiwa na changamoto za kipato. Tunaamini elimu ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema Tracy.

Aliongeza kuwa taarifa zote kuhusu udahili, kozi zinazotolewa na taratibu za kujiunga na chuo hicho zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya KIUT ya www.kiut.ac.tz

KIUT ni tawi la Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala kilichoanzishwa nchini Uganda mwaka 2001. Nchini Tanzania, taasisi hiyo ilianza mwaka 2008 kama chuo kishiriki cha Dar es Salaam (KIU-DCC) chini ya Kampala International University.

Mnamo Januari 15, 2011, chuo hicho kilipata usajili wa muda kutoka Tume ya chuo kikuu Tanzania (TCU), kabla ya kupewa usajili kamili tarehe 27 Septemba 2012. Baadaye, tarehe 17 Julai 2017, TCU ilikipa hadhi ya kuwa chuo kikuu kamili kwa jina la Kampala International University in Tanzania (KIUT).

Kutokana na ubora wa huduma za elimu zinazotolewa, tarehe 2 Agosti 2022 chuo hicho kilitunukiwa cheti cha ithibati, hatua iliyothibitisha kukidhi viwango vinavyohitajika katika utoaji wa elimu ya juu nchini.

Kwa sasa, KIUT ambacho kwa Tanzania kiko eneo la Gongo la Mboto Jijini Dar es salaam, ni miongoni mwa vyuo vikuu vinavyotoa programu mbalimbali zinazolenga kukidhi mahitaji ya maendeleo ya jamii katika nyanja tofauti, zikiwemo Sayansi za Jamii, Uhandisi, Kilimo, Sheria, Sayansi za Afya, Biashara, Elimu pamoja na Sayansi na Teknolojia.

 

Post a Comment

0 Comments