RC MHITA AWAAGIZA VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA KUSIMAMIA SUALA LA USAFI WA MAZINGIRA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewaagiza viongozi wa Serikali za mitaa kuhakikisha zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi linatekelezwa kwa ufanisi, huku akitaka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuchukua tahadhari mapema kutokana na matarajio ya mvua za El Niño.

Mhita ametoa maagizo hayo leo, Septemba 25, 2026, wakati akiwaongoza viongozi wa mkoa na wilaya pamoja na wananchi katika uzinduzi wa Kampeni maalum ya usafi wa Mazingira, uliofanyika katika Soko la Ujasiriamali la Ibinzamata, mjini Shinyanga.

Mhita amebainisha kuwa, siku ya Jumamosi imeainishwa kuwa siku maalumu ya usafi kuanzia ngazi ya kaya, ambapo viongozi wa Serikali za mitaa wanapaswa kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo kwenye maeneo yao.

Aidha, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Shinyanga kuwasilisha tathmini za kila mwezi kuhusu hali ya usafi katika kata na maeneo mbalimbali, hatua ambayo itasaidia kubaini maeneo yenye changamoto na kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwatoza faini wale wasiozingatia kanuni za usafi.

Katika hatua nyingine, Mhita amewataka wananchi wanaoishi mabondeni na maeneo hatarishi kuchukua tahadhari mapema kutokana na matarajio ya mvua za El Niño, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka za Serikali.

Amesema wananchi wanapaswa kuhama maeneo hatarishi endapo wataelekezwa kufanya hivyo, ili kulinda maisha ya watu na kuepusha madhara kwa miundombinu.

Mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga amebainisha kuwa, Serikali imeendelea kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, ameahidiki suala la usafi kusimamiwa kikamilifu katika wilaya yake ambapo amewataka wananchi, viongozi na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo ya usafi wa mazingira iliyozinduliwa leo na Mkuu wa mkoa  ili kufikia malengo yanayotarjiwa.

Post a Comment

0 Comments