TLS SHINYANGA YABAINISHA NAMNA INAVYOWEZA KUTOA MSAADA WA KISHERIA KWA WATU WASIOKUWA NA UWEZO



Mwenyekiti wa TLS mikoa ya Shinyanga na Simiyu, Wakili Shaban Mvungi

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, kimeeleza namna watu wasio na uwezo wa kifedha wanavyoweza kupata msaada wa kisheria bila malipo, ikiwemo uwakilishi na utetezi mahakamani.

Mwenyekiti wa TLS katika mikoa hiyo, Wakili Shaban Mvungi, amesema chama hicho kupitia mawakili wa kujitegemea kinaweza kutoa msaada wa kisheria kwa mtu mwenye kesi mahakamani endapo, baada ya kufanyiwa tathmini, itabainika kuwa hana uwezo wa kumudu gharama za huduma ya wakili na kesi yake inahitaji uwakilishi wa kisheria.

Amesema mwananchi anayehitaji msaada huo anaweza kuwasiliana moja kwa moja na uongozi wa TLS au kupitia mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria. 

TLS hufanya ufuatiliaji na tathmini ya hali ya mhusika kabla ya kutoa huduma hiyo, ili kujiridhisha kuwa anakidhi vigezo vya kupata msaada wa kisheria bila malipo.

Wakili Mvungi amesema, TLS pia kwa kushirikiana na wadau wengine, hutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu walioko magerezani kupitia taratibu maalum zinazotambuliwa na sheria.

Aidha, amesema TLS Makao Makuu inaweza kuwawekea mawakili watuhumiwa wanaokabiliwa na makosa makubwa yenye adhabu kali, yakiwemo makosa ya uhaini na uhujumu uchumi, pale ambapo masharti ya kisheria yanapotimizwa.

Wakili Mvungi, ambaye ni wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya Mawakili ya MS & CO. LAW ATTORNEYS iliyopo mjini Shinyanga, amesema Mahakama Kuu pia ina mamlaka ya kumteua wakili wa kujitegemea kumwakilisha mtuhumiwa katika makosa makubwa, yakiwemo mauaji na uhaini, kwa kuzingatia masharti ya sheria.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mawakili, Sura ya 341, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, kifungu cha 49, wakili mwenye cheti halali cha uwakili anaweza kufanya kazi ya uwakili katika Mahakama Kuu na mahakama zilizo chini yake.

Aidha, kifungu cha 63 kinampa mtuhumiwa au mlalamikaji haki ya kumwajiri wakili binafsi kwa ajili ya kumwakilisha au kumtetea mahakamani kwa malipo ya ada.

Hata hivyo, Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 21, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, imeweka mfumo wa kuhakikisha watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria wanapata msaada unaostahili.

Kwa mujibu wa kifungu cha 33(1) cha sheria hiyo, Mahakama inaweza kuamuru mtuhumiwa wa kosa la jinai apewe msaada wa kisheria kupitia wakili wa kujitegemea endapo itajiridhisha kuwa, hana uwezo wa kifedha wa kupata huduma ya wakili na kwamba, maslahi ya haki yanahitaji awe na wakili katika utetezi au rufaa ya kesi inayomkabili.

Kifungu cha 33(3) kinaeleza kuwa, wakili anayeteuliwa na Mahakama kumtetea mtuhumiwa hulipwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mahakama.

Aidha, kwa watuhumiwa wanaokabiliwa na kesi za jinai za mauaji na uhaini, ambazo zinaweza kubeba adhabu ya kifo, msaada wa kisheria hutolewa moja kwa moja kwa gharama za Serikali kupitia utaratibu unaotambuliwa kisheria.

Kwa ujumla, mtu anayehitaji uwakilishi au utetezi wa kisheria mahakamani anaweza kupata huduma hiyo kupitia njia kuu tatu. 

Kwanza, anaweza kumwajiri wakili binafsi kwa malipo ya ada. 

Pili, anaweza kupangiwa wakili kupitia utaratibu wa msaada wa kisheria wa Mahakama endapo atakidhi vigezo vilivyowekwa na sheria. 

Tatu, anaweza kupata msaada wa kisheria bila malipo kutoka kwa watoa huduma za msaada wa kisheria, wakiwemo mawakili wa kujitegemea, endapo atakidhi masharti yaliyowekwa.

 

Post a Comment

0 Comments