RC SHINYANGA AZITAKA KAMATI ZA MAAFA KUJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amezitaka idara na tasisi za Serikali zinazounda Kamati za maafa kwenye wilaya na mkoa kujipanga kikamilifu, ili kukabiliana na athari za mvua za El nino, zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwishoni mwa mwezi huu.

Mhita ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao cha mkoa cha kamati za maafa , kilichowakutanisha wakuu wa idara na tasisi za Serikali kutoka mkoa na wilaya, kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kutokea wakati wa mvua za vuli, ambazo zinahofiwa kuwa juu ya wastani, ikiwemo kusababisha mafuriko.

Amewaagiza wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanaongoza kamati hizo za maafa kwenye wilaya na kusimamia mipango na mikakati yote iliyowekwa, ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea na kwamba, timu ya maafa ya mkoa itakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na timu za wilaya.

Mhita, amezitaka mamlaka zinazohusika na miundombinu ya barabara ikiwemo TANROADS na TARURA, kuhakikisha miundombinu ya barabara inaboreshwa, huku shirika la umeme Tanesco na Mamlaka zinazosimamia huduma za maji katika mkoa za RUWASA, KUWASA, KASHWASA na SHUWASA, kujipanga katika kukabiliana na mazingira yoyote yatakayoathiri utoaji wa huduma.

Mkuu huyo wa mkoa pia ameiagiza idara ya afya kufanya tathmini na kuandaa  dawa na vifaa tiba  kwa ajili ya huduma za dharura, ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kutolea huduma kwa wathirika.

Pia, amelitaka shirika la Msalaba mwekundu kujipanga katika kuratibu timu za ukoaji na waathirika, ikiwemo utoaji wa huduma za kisaikolojia kwa wale watakaokumbwa na changamoto.

Halikadhalika, amezitaka Tume za madini katika mikoa ya kimadini ya Shinyanga na Kahama, kuhakikisha hali ya usalama wa miundombinu inaimarishwa kwenye maeneo yote ya uchimbaji, ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea wakati mvua hizo zitakapoanza kunyesha.

Akizungumzia sekta ya kilimo amesema, wataalam wa Sekta hiyo wanapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu kulima mazao yanayoweza kustahilmili hali hiyo ya mvua, ili kuepuka changamoto ya upungufu wa chakula katika siku za usoni.

Mbali na hatua hizo, Mhita pia emeelekeza elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi ili wafahamu namna ya kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo sehemu ya kutoa taarifa kwa ajili ya kupata msaada pale wanapopatwa na changamoto yoyote.

Kikao hicho ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa wa Shinyanga, kimewakutanisha wakuu wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali, wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri na Kamati nzima ya ulinzi na usalama ya mkoa.


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita

Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Bi. Pili Mnyema
Katibu wa kamati ya maafa mkoa wa Shinyanga Bw.Alex Mpasa ambaye pia ni Katibu Tawala msaidizi Mipango na Uratibu mkoa
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Peter Masindi
Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga
Wakuu wa Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali wanaounda kamati za maafa kwenye mkoa na Wilaya

 

Post a Comment

0 Comments