
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara, wananchi wa kata hiyo walimuomba Kamanda huyo kuona namna ya kuwawekea kituo cha Polisi katika eneo eneo lao, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kipolisi karibu na makazi yao.
Pamoja na
mambo mengine, wananchi hao pia waliomba ufafanuzi kuhusu utaratibu wa dhamana
kwa watuhumiwa wa makosa yenye dhamana, ambapo Kamanda Magomi alifafanua kuwa, dhamana
inapaswa kutolewa bila malipo kwa makosa yote yanayodhaminika.
Kamanda
Magomi aliwataka wananchi kutotoa fedha yoyote wakati wa kuwadhamini ndugu zao, na
badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa juu wa polisi ikiwemo
Ofisini kwake, pale wanapoona viashiria vya kuombwa fedha na polisi wasio waminifu ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Kuhusu ombi
la wananchi la kujengewa kituo cha Polisi amebainisha kuwa, amelichukua suala hilo kwa uzito unaostahili, na atalishughulikia kwa kushirikiana na mamlaka nyingine wakiwemo wananchi wenyewe.
Aidha, Kamanda Magomi ametumia kikao hicho kutoa elimu kuhusu dhana ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kudhibiti vitendo vya uhalifu, kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu na matukio ya uhalifu.
Amewasisitiza wananchi kutowalinda au kuwaficha wahalifu, badala yake wachukue hatua ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kutoa ushahidi pale wanaposhuhudia vitendo hivyo, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pia amewasihi wazazi na walezi kutambua wajibu wao wa kuwalea na kuwaongoza watoto kwa kuzingatia misingi ya maadili mema, akieleza kuwa, malezi bora ni msingi muhimu wa kuandaa raia wema na kujenga jamii itakayowezesha kuwa na taifa imara kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Wakati huohuo, Kamanda Magomi amewakumbusha wananchi kujiandaa na kuchukua tahadhari za kiusalama kabla na wakati wa mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.



0 Comments