SAVANNAH PLAINS SCHOOLS KUWEKEZA KATIKA MAFUNZO YA VITENDO KUKUZA UBUNIFU NA UWEZO WA KITAALUMA KWA WANAFUNZI

 

Shule ya Savannah Plains Schools iliyopo Manispaa ya Shinyanga, imeahidi kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa madarasa ya awali na msingi, hatua inayolenga kuwajengea uwezo na kuwaandaa kuwa wabobevu katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Ahadi hiyo imetolewa Ijumaa tarehe 18, Septemba, 2026, na Mwalimu Mkuu ya shule ya awali na msingi wa shule hiyo, Wema Kanyika, wakati akizungumza katika mahafali ya kwanza ya darasa la Saba, tangu shule hiyo ianze kutumia mtaala wa ndani na mahafali ya tatu kwa wanafunzi wa darasa la Awali.

Mwalimu Mkuu wa shule ya awali na msingi Savannah Plains schools Wema Kanyika

Kanyika amesema shule imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayowawezesha kuelewa na kutumia maarifa kwa vitendo, badala ya kujikita katika maandalizi ya mitihani pekee.

Amesema lengo la shule hiyo ni kuwajenga wanafunzi kuwa wabunifu na wenye uwezo wa kutumia maarifa kutatua changamoto mbalimbali , pamoja na kuendana na mabadiliko ya dunia katika nyanja za sayansi na teknolojia.

“Hatufundishi watoto kwa ajili ya mitihani pekee, bali tunawaandaa kuwa wabunifu na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohitaji maarifa na ujuzi,” amesema Kanyika.

Aidha, Kanyika amesema pamoja na shule hiyo kufundisha kwa kufuata mtaala wa ndani, ina mpango wa kuanza kufundisha lugha ya Kichina kuanzia mwaka 2027, hatua ambayo inalenga kuwapa wanafunzi ujuzi wa ziada wa mawasiliano na kuwaongezea fursa katika nyanja mbalimbali za kimataifa.

Akizungumzia matokeo ya mitihani ya kitaifa, amesema tangu shule hiyo ianze kutumia mtaala wa ndani mwaka 2024, wanafunzi wote waliofanya mtihani wa Darasa la Nne katika kipindi cha mwaka 2024 na mwaka 2025, walipata daraja A, hali ambayo inawapa uhakika wa kupata matokeo mazuri katika mtihani wa darasa la saba kwa mwaka huu.

Kwa upande wake, Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Dkt. Paschal Shiluka, amepongeza uongozi wa Savannah Plains Schools kwa kuwekeza katika mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, akisema hatua hiyo inawapa wanafunzi motisha ya kusoma kwa bidii na kuimarisha maendeleo yao ya kitaaluma.

Dkt. Paschal Shiluka

Dkt. Shiluka, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo na Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, amesema uwekezaji uliofanywa na shule hiyo unaonesha dhamira ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora inayowaandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Amesema uwekezaji huo unajumuisha maabara za kisasa na vifaa mbalimbali vya kujifunzia, vinavyowawezesha wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo, pamoja na ziara za kielimu zinazolenga kuwaongezea ujuzi na kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu.

Aidha, amesema hatua ya shule hiyo kuwashirikisha wanafunzi katika mashindano ya kitaifa na kimataifa yanayohusisha masuala mbalimbali ya kitaaluma ikiwemo mijadala, ubunifu na teknolojia, inawasaidia kukuza vipaji na uwezo wao, hatua ambayo italiwezesha taifa kupata wataalam wazuri.

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 13 wamehitimu elimu ya msingi, huku wanafunzi 64 wakihitimu elimu ya awali.

Savannah Plains Schools ambayo ni shule binafsi inayomilikiwa na mwekezaji mzawa, ilianzishwa mwaka 2013 kwa kutumia mtaala wa kimataifa wa Cambridge, ambapo mwaka 2024 iliachana na mtaala huo na kuanza kutumia mtaala wa ndani unaosimamiwa na Baraza la Mitihani la taifa (NECTA).

Shule hiyo inayotumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia, pia ina miundombinu ya kisasa ya kujifunzia ambayo inakwenda pamoja na kutoa huduma mbalimbali kwa wanafunzi  ikiwemo za afya kupitia zahanati iliyopo shuleni hapo, inayohudumiwa wataalamu Afya akiwemo daktari, muuguzi na mtaalamu wa huduma za maabara.

Pia, ina kitengo maalum cha mafunzo ya michezo ambacho kinawawezesha wanafunzi kukuza vipaji vyao katika upande wa mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu na kuogelea na ina mahusiano na taasisi mbalimbali za kielimu ndani na nje ya nchi ambazo inashirikiana nazo katika kuwasaidia wanafunzi kukuza uwezo wao wa kitaaluma.

Savannah Plains Schools pia inajumuisha elimu ya Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, ambapo kwa upande wa elimu ya awali na msingi kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 558.
Wahitimu darasa la saba
Baadhi ya wahitimu darasa la awali
Baadhi ya wahitimu darasa la awali
Wawakilishi wa wahitimu wakisoma risala kwa mgeni rasmi
MC Tumaini Chiwa aliyekuwa akisherehesha wa sherehe za Mahafali 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya shule
Meza kuu wakifuatilia matukio mbalimbali kwenye sherehe za mahafali
Mgeni rasmi na Wajumbe wa Kamati ya shule wakiwa mbele kwa ajili ya kushiriki zoezi la kukata keki

Dr. Paschal Shiluka akiwa tayari kuongoza zoezi la kukata keki kwa kushirikiana na Mwalimu mkuu Bi. Wema Kanyika pamoja na wawakilishi wa wahitimu
Wajumbe wa Kamati ya shule
Wazazi na watu mbalimbali wakiwa kenye sherehe za mahafali

 


Post a Comment

0 Comments