WATU 12 WAKIWEMO ASKARI WATANO WAMEPOTEZA MAISHA KWA AJALI YA GARI MKOANI SINGIDA

Watu 12 wamefariki dunia, wakiwemo askari watano wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida na mahabusu saba, katika ajali iliyotokea eneo la Mlima Sekenke, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea leo, Septemba 21, 2026, majira ya saa 1:45 asubuhi katika barabara kuu ya Singida–Nzega, eneo la Mlima Sekenke, Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo.
Amewataja Askari waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na Mkuu wa Kituo cha Polisi Shelui wilayani Iramba mkoani Singida, SP Frank Lazima Mwasapili. 
Mbali na SP Mwasapili, askari wengine waliofariki ni S/SGT Ussi Hassan, SGT Paulo Silivin Gabriel, PC Ashraf Salumu Kheri na PC Nangida Ramadhani Mushi, ambao wote walikuwa wakitumika katika Kituo cha Polisi Shelui.
Ajali hiyo pia imesababisha vifo vya mahabusu saba, ambao walikuwa wakisafirishwa kwa gari hilo la polisi kutoka kituo cha Polisi Shelui kwenda Mahakama ya Wilaya.
Kwa mujibu wa Kamanda Kakwale, ajali hiyo ilihusisha lori lenye namba za usajili RAF 243X/TRL 4255, mali ya Kampuni ya YYUSSA ya Kigali, Rwanda, na gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba PT 1982, mali ya Jeshi la Polisi Tanzania ambalo liligongwa na lori na kutumbukia korongoni katika eneo hilo la Mlima Sekenke.
SOURCE: IPP MEDIA

Post a Comment

0 Comments