TANESCO SHINYANGA YAKABIDHI MSAADA KWA WATOTO WANAOTOKA KWENYE MAZINGIRA HATARISHI

 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga, limekabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi, wanaolelewa kwenye Kituo cha AGAPE, kilichopo  Chibe Manispaa ya Shinyanga.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Mteja wa shirika hilo mkoani Shinyanga, Julius Minja, amesema msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, pamoja na kutekeleza wajibu wa shirika kwa jamii (CSR).

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Mteja TANESCO mkoa wa Shinyanga, Julius Minja

Minja amesema TANESCO imeamua kuwafikia watoto hao baada ya kutambua mahitaji na changamoto wanazokabiliana nazo, hivyo kuona umuhimu wa kushirikiana na jamii katika kuwasaidia.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Rasilimali Watu wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Rehema Juma, amesema shirika hilo limeguswa na hali ya watoto hao na kuamua kuwapatia msaada ili nao waweze kufurahia na kupata mahitaji muhimu kama watoto wengine.

Kaimu Afisa Rasilimali Watu wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, (Aliyefunika kichwa kwa kitambaa cha njano) Rehema Juma

Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo, watoto hao wameishukuru TANESCO Mkoa wa Shinyanga kwa kuwafikiria na kuguswa na mahitaji yao, huku wakiiomba jamii na wadau wengine kuendelea kuwasaidia.

Aidha, watoto hao wamelishukuru shirika hilo kwa kuwaunganishia huduma ya umeme huku wakibainisha kuwa, hatua hiyo imewaondolea changamoto ya muda mrefu ya kutegemea umeme wa jua ambao haukuwa wa uhakika, hali ambayo iliwafanya washindwe kujisomea wakati wa usiku, kutokana na umeme huo wa jua kuwaka kwa muda mfupi na baadaye kuzima, kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu.

Pamoja na msaada huo, watoto hao wamesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni upungufu wa chakula na mahitaji mengine muhimu, ikiwemo vifaa vya shule, pamoja na ukosefu wa fedha za kununulia umeme wa LUKU.

Wamesema licha ya juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. John Myola kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu, bado kuna baadhi ya mahitaji ambayo imekuwa vigumu kuyatimiza kutokana na kutumia muda mwingi kushughulikia changamoto ya kiafya inayomkabili.

Kufuatia msaada huo, Mkurugenzi wa Kituo hicho cha AGAPE, John Myola, ameushukuru uongozi wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto hao.

Mkurugenzi wa Kituo cha AGAPE, Bw. John Myola,

Myola amesema kwa sasa kituo hicho hakina mfadhili maalum na badala yake kinategemea zaidi misaada kutoka kwa jamii pamoja na baadhi ya taasisi za dini ambazo zimekuwa zikiwasaidia.

Amesema misaada inayotolewa bado haikidhi ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo, hivyo amewaomba watu binafsi, taasisi za Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kukishika mkono kituo hicho, ili kiweze kuwahudumia watoto hao kwa ufanisi.

Myola amebainisha kuwa, kwa sasa kituo hicho kinalea jumla ya watoto 37 wanaosoma shule za Msingi na Sekondari, pamoja na watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano na kwamba, licha ya changamoto wanazokabiliana nazo,  wanaona kuishi katika kituo hicho ni salama zaidi kuliko mazingira waliyotoka, ambayo ni hatarishi zaidi.

Msaada uliotolewa na TANESCO katika kituo hicho ni pamoja na mchele kilogramu 100, unga wa sembe kilogramu 100, maharage kilogramu 50, sukari kilogramu 25 na lita 20 za mafuta ya kupikia.

Misaada iliyotolewa
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Mteja TANESCO mkoa wa Shinyanga, Julius Minja akizungumza na Mkurugenzi wa kituo cha AGAPE Bw.John Myola

Baadhi ya watumishi wa TANESCO mkoa wa Shinyanga waliomwakilisha Meneja wa Shirika hilo Mhandisi Hadija Mborouk
Mkurugenzi wa Kituo cha AGAPE John Myola akiwatembeza wageni kwenye maeneo mbalimbali ya kituo hicho

Post a Comment

0 Comments