Ndege ya majaribio imefanikiwa kutua na kuruka katika Uwanja
wa Ndege wa Shinyanga leo Juni 12, 2026, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuanza
kwa huduma rasmi za usafiri wa anga kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo jirani.
Baada ya majaribio hayo yaliyohusisha ndege iliyowasili
kutoka Uwanja wa Ndege wa Musoma baada ya hapo iliruka kuelekea Dodoma.
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, akizungumza
kwenye hafla hiyo, ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya kazi
usiku na mchana kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika kwa asilimia 100
ifikapo Septemba 1 mwaka huu ,ili ndege za abiria zianze kutua na kutoa huduma.
Profesa Mbarawa amesema anaufahamu mradi huo tangu ulipoanza
kutekelezwa alipokuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akisisitiza
kuwa ni lazima ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Amesema viwanja vya ndege vya Tabora, Sumbawanga na Kigoma
tayari vimekamilika, hivyo hakuna sababu ya Uwanja wa Ndege wa Shinyanga
kuchelewa kukamilika.
Aidha, amesema ujenzi wa uwanja huo pamoja na miradi mingine
ya viwanja vya ndege nchini unalenga kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga,
kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji
pamoja na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita,
amesema kukamilika kwa uwanja huo kutakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa
uchumi wa mkoa kwa kuwezesha usafiri wa haraka wa watu na mizigo pamoja na
kuvutia wawekezaji.
Naye Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS Mhandisi Japherson
Nnko, amesema mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga ulianza Aprili
2023 na ulipitia changamoto zilizochelewesha utekelezaji wake kwa muda.
Amesema mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni 45 sasa
umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika ifikapo
Agosti 30, 2026, tayari kwa kuanza kutoa huduma za ndege za abiria kuanzia
Septemba 1 mwaka huu.
0 Comments