MARIDHIANO YA KWELI YANAHITAJI HEKIMA, WELEDI NA MAZUNGUMZO YENYE MAANA

 

Taifa letu linaendelea na mijadala mbalimbali inayolenga kuwaleta Watanzania pamoja, hasa kutokana na changamoto mbalimbali ambazo tumepitia, ikiwemo makovu ya uchaguzi na migongano ya kimaslahi inayotokana na tofauti zetu za kifikra, kimtazamo na kiitikadi.

Ninaunga mkono kwa asilimia mia moja wito wa maridhiano. 

Hata hivyo, kabla ya kuzungumza kuhusu maridhiano, ni muhimu kujiuliza maswali ya msingi: Kwa nini tunahitaji maridhiano? Nini kimesababisha tufikie hatua hii? Tukiridhiana, tunataka kufikia nini? Je, sababu zilizotufikisha hapa zinafahamika na kukubalika na pande zote? Na je, tuko tayari kuzitafutia ufumbuzi?

Aidha, tunapaswa kujiuliza ni nani watakaokaa kwenye meza ya mazungumzo, nani atasimamia mchakato huo na kwa maslahi ya nani.

Ikiwa wananchi ndio kipaumbele, watashirikishwa kwa namna gani? Watapata nafasi ya kuwasilisha maoni yao moja kwa moja au watawakilishwa? Na kama watawakilishwa, je, watawakilishwa na nani? wana imani na wawakilishi wao kwamba watasimamia ipasavyo maslahi yao?

Haya si maswali ya kupuuzwa. Ni maswali ambayo majibu yake yanaweza kusaidia kujenga msingi wa maridhiano ya kweli, yenye kuaminika na yenye uwezo wa kulivusha taifa kutoka kwenye changamoto tulizonazo.

Maridhiano yasiwe Ajenda ya upande mmoja

Tunapaswa pia kujiuliza: Ni nani anayesukuma ajenda ya maridhiano? Je, anayesukuma ajenda hiyo anaelewa hisia, hofu na matarajio ya wale anaotaka kukaa nao katika meza ya mazungumzo? Ana uwezo wa kuwasikiliza na kuwasiliana nao kwa lugha inayojenga uaminifu?

Maridhiano hayawezi kujengwa kwa kauli kali, mashambulizi, lawama au kutafuta ushindi wa upande mmoja. Yanahitaji watu wenye uwezo wa kusikiliza, kuelewa mitazamo tofauti na kutafuta eneo la pamoja.

Kwa sababu hiyo, suala la maridhiano halipaswi kuachwa kwa waropokaji, wachambuzi wanaotafuta umaarufu, au watu wanaotumia mijadala ya kitaifa kulinda maslahi yao binafsi au ya upande fulani.
Wapo wanaoweza kuonekana kana kwamba wanasaidia kujenga maridhiano, lakini kwa kauli na mwenendo wao wanazidi kuwagawa Watanzania.

Serikali itumie watu wenye weledi kujibu Hoja nzito

Ni wakati pia kwa mamlaka husika kukomesha utamaduni wa kila mtu kuitisha vyombo vya habari na kujibu hoja zinazoelekezwa kwa Serikali, hususan katika masuala nyeti na muhimu kwa taifa.

Hali hii imekuwa ikichochea mijadala isiyo na tija, kwa sababu baadhi ya wananchi huamini kuwa mtu anayejibu hoja kwa namna hiyo ametumwa na mamlaka. Hatimaye, badala ya hoja kujibiwa kwa weledi, mjadala hugeuka kuwa mvutano unaozalisha mgawanyiko zaidi.

Tunaamini Serikali ina watu wenye uwezo mkubwa: wasomi, wataalamu, viongozi na watu wenye uelewa mpana wa masuala ya kitaifa. Kwa nini basi isiwatumie watu wenye weledi, uaminifu, ushawishi, uwezo wa kujenga hoja, wanaojua mbinu za kuwasiliana na umma na wenye uelewa wa hisia za wananchi?

Mambo mazito yanahitaji watu wenye uwezo unaolingana na uzito wa hoja hizo. Si kila mtu anaweza kujibu kila hoja. 

Hoja nzito inapowasilishwa na mtaalamu au msomi, inapaswa kujibiwa na mtu mwenye uelewa, maarifa na uwezo wa kujenga hoja kwa kiwango kinacholingana na hoja hiyo.
Kwa mfano, si kila mtu anaweza kujibu hoja iliyotolewa na Profesa Anna Tibaijuka. Hoja ya kiwango hicho inahitaji mjibu hoja mwenye sifa, maarifa na uzoefu unaolingana nayo. 

Serikali isiruhusu watu wasio na sifa wala mamlaka kutoa majibu yanayoweza kuathiri taswira ya Serikali au kuendeleza mgawanyiko katika jamii.

Tupime kauli zetu

Pamoja na hayo, ni muhimu kila mmoja wetu ajifunze kupima kauli anazotoa katika mijadala ya kitaifa. Kabla ya kuzungumza, tunapaswa kujiuliza: Kauli yangu inajenga au inabomoa? Inasaidia kuleta watu pamoja au inazidi kuwagawa?

Haiwezi kuwa na maana mtu akidai anaitetea Serikali, lakini wakati huo huo anashambulia taasisi nyingine, viongozi wa dini au makundi ya wananchi kwa kuamini kwamba kufanya hivyo kutaisaidia Serikali.

Ulinzi wa maslahi ya taifa haujengwi kwa kuwashambulia wengine. Unajengwa kwa hoja, heshima, busara, ukweli na uwezo wa kuzungumza na watu wenye mitazamo tofauti.

Maridhiano ya kweli yanahitaji ujasiri wa kusikiliza

Tanzania inahitaji maridhiano, lakini zaidi ya yote inahitaji maridhiano ya kweli, yenye malengo yanayoeleweka, yanayoshirikisha pande husika na yanayolenga kutatua chanzo cha migogoro, si kuficha matatizo yaliyopo.

Maridhiano ya kweli hayawezi kujengwa kwa propaganda, mashambulizi ya kisiasa, kauli za jazba wala kwa kuwanyamazisha wanaotofautiana nasi. 

Yanahitaji uaminifu, kusikilizana, kuheshimiana na utayari wa kila upande kukubali kwamba taifa ni kubwa kuliko maslahi ya mtu, kundi au chama.
Ikiwa tunataka kuvuka tulipo, basi tuanze kwa kujibu maswali magumu, kuwashirikisha wahusika, kutumia watu wenye weledi na kuhakikisha kila kauli inayotolewa inalenga kujenga, si kubomoa.

Taifa linahitaji maridhiano. Lakini maridhiano hayo yatafanikiwa pale tutakapokuwa tayari si tu kuzungumza, bali pia kusikilizana, kuelewana na kuchukua hatua za kushughulikia sababu zilizotufikisha hapa.

Tanbihi: Picha zilizotumika kwenye maoni haya siyo halisi, bali zimetengenezwa kwa lengo la kusaidia kufikisha ujumbe. 

Post a Comment

0 Comments