Lyamongi, ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi
anayeshughulikia Raslimali Watu na Utawala, amesema hatua hiyo itasaidia
mashirika hayo kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali, hata pale wafadhili
wanapositisha ufadhili.
Amesema mashirika mengi yamekuwa yakishindwa kuendeleza
miradi yaliyoianzisha kutokana na utegemezi mkubwa wa ufadhili kutoka nje ya
nchi, ikiwemo mataifa ya Ulaya, wakati wafadhili hao wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto mbalimbali, zikiwemo kuweka masharti mapya na magumu au kusitisha
kabisa ufadhili.
Kutokana na hali hiyo, Lyamongi ameyataka mashirika hayo
kuanzisha shughuli za uzalishaji zinazoendana na malengo yao, ili kupata mapato
ya kusaidia gharama za uendeshaji na utekelezaji wa miradi.
Aidha, ameyapongeza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa
mchango mkubwa yanayoutoa katika maendeleo ya nchi, akisema yamekuwa wadau
muhimu wa Serikali kwa miaka mingi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika
Sekta ya afya, elimu, uwezeshaji wa wanawake na vijana, mazingira, haki za
binadamu, ustawi wa jamii, kupunguza umaskini na kuongeza fursa za kiuchumi.
Ameyataka mashirika hayo kuhakikisha mipango na utekelezaji wa shughuli zao unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kuimarisha ustawi na maendeleo ya taifa.
Akifafanua suala hilo, Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga, Focus Magobe, amesema
shughuli hizo hazipaswi kuwa na lengo la kibiashara, bali zijikite katika kusaidia
mashirika kuendeleza shughuli zao.
Ametolea mfano wa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali yanayoisaidia jamii kuingiza kipato ambazo hazitozwi kodi, akisema uzalishaji wake unahesabika kuwa uko kwa ajili ya kujikimu, na hauchukuliwi kama wenye malengo ya kibiashara.
Naye Mwakilishi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) Mkoa wa Shinyanga, Juma Bakari, amesema baraza hilo limechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto za kiutendaji zinazoyakabili mashirika hayo.
Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuyakutanisha mashirika na mamlaka za Serikali, ikiwemo TRA, ili kupata maelekezo kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, amesema NACONGO inaendelea na mchakato wa kuanzisha mitandao ya NGOs katika kila wilaya.
Kupitia jukwaa hilo, wadau mbalimbali walitoa elimu kuhusu
masuala yanayohusu utekelezaji wa shughuli za NGOs.
TRA ilitoa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na
taratibu za kodi, huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
ikieleza umuhimu wa uwazi, maadili na uzalendo katika utekelezaji wa shughuli
za mashirika hayo.
Idara ya Uhamiaji ilitoa ufafanuzi kuhusu vigezo na
taratibu za kupata vibali vya kuajiri raia wa kigeni, wakati Shirika la World
Vision lilitoa mafunzo kuhusu mbinu za uandishi wa maandiko ya miradi (Project
Proposals).
Kwa upande wake, Idara ya Maendeleo ya Jamii iliwasilisha
taarifa kuhusu hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoani Shinyanga na
kueleza nafasi ya NGOs katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Kaulimbiu ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mwaka huu inasema: “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.”
0 Comments