FAHAMU TARATIBU ZA KUFUNGUA KESI MAHAKAMA KUU

Mahakama kuu ya Tanzania, imepewa mamlaka ya kusikiliza na kutoa maamuzi ya mashauri mbalimbali, chini ya Ibara ya 107A, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mashauri yanayosikilizwa na kutolewa maamuzi katika mahakama hiyo, ni pamoja na mapya yaliyoelekezwa na sheria kufunguliwa moja kwa moja katika mahakama hiyo, pamoja na yale yaliyokatiwa rufaa kutoka katika Mahakama za chini. Mamlaka hayo, yamebainishwa zaidi katika Ibara ya 108(1) na 108(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kutokana na maboresho makubwa ya utoaji ya huduma  yaliyofanywa na Mahakama, kwa sasa mikoa yote nchini ina Mahakama kuu, isipokuwa mkoa mmoja tu wa Pwani, ambao unatajwa kutokuwa na Mahakama hiyo kutokana na  mwingiliano wa kijiografia uliopo kati yake na mkoa wa Dar es salaam. 

Kabla ya maboresho hayo, Mahakama kuu zilizokuwa katika mikoa michache  zililazimika kuunda kanda iliyojumuisha mikoa kadhaa, hatua ambayo iliwalazimu Majaji kusikiliza mashauri kutoka katika mikoa zaidi ya mitatu hali ambayo ilisababisha mashauri kuchukua muda mrefu, huku wananchi wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama.

Hali hiyo ilitokana na upungufu wa Majaji pamoja na kutokuwepo kwa miundombinu iliyowezesha kuanzishwa kwa Mahakama hiyo kwenye mikoa, jambo ambalo lilitatuliwa miaka michache iliyopita, baada ya Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa Mahakama nchini kuanza ujenzi wa Mahakama kuu kwenye kila mkoa, na marais kwa nyakati tofauti kuteua Majaji kwa mujibu wa sheria, ambao kwa sasa wanahudumu katika Mahakama hizo.

Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Shinyanga ni kati ya zao la Mkakati huo wa kusogeza huduma za kimahakama kwa wananchi, ambayo kwa sasa inahudumiwa na Majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Shinyanga Mheshimiwa John Kahyoza.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Shinyanga Mheshimiwa John Kahyoza

Majaji wengine wanaohudumia Mahakama hiyo ni Mheshimiwa Ruth Massam na Mheshmimiwa Ntuli Mwakahesya.

Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Shinyanga Mheshimiwa Ntuli Mwakahesya

SHINYANGA ONE MEDIA imetembelea Mahakama hiyo kwa lengo la kujua endapo wananchi wana uelewa wa kutosha kuhusu uhuhimu wa uwepo wake, pamoja na utaratibu wa kuifikia na namna ya kufungua mashauri.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Shinyanga, Mheshimiwa Gadiel Mariki, amesema pamoja na uwepo wa Mahakama kuu katika kila mkoa ukiwemo mkoa wa Shinyanga, bado baadhi ya wananchi hawafahamu utaratibu wa kufungua mashauri katika Mahakama hiyo kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya kisheria, hali inayowafanya baadhi yao kujiweka mbali na chombo hicho cha haki .

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Shinyanga, Mheshimiwa Gadiel Mariki

Amesema hivi sasa Mahakama hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya kujenga uelewa kwa wananchi, ikiwemo kutoa elimu kupitia matukio mbalimbali ya kimahakama na kwenye vyombo vya Habari, ili wananchi wakione chombo hicho kuwa kiko kwa ajili ya kuwawezesha kupata haki zao.

Mheshimiwa Mariki amebainisha kuwa, hivi sasa mwananchi anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania bila kulazimika kufika Mahakamani, baada ya maboresho ya mfumo wa uendeshaji wa mashauri kuwezesha huduma hizo kupatikana kwa njia ya mtandao.

 Amesema tangu mwaka 2023, mashauri yote katika Mahakama hiyo yanafunguliwa kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (e-CMS).

Amesema mfumo huo ni sehemu ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Mahakama nchini, yaliyokwenda pamoja na kusogeza huduma za Mahakama Kuu karibu na wananchi kwa kujenga Mahakama Kuu katika kila mkoa.

Mheshimiwa Mariki ameendelea kufafanua kuwa, mwananchi mwenye akaunti katika mfumo wa e-CMS anaweza kufungua shauri akiwa mahali popote kupitia mtandao, bila kulazimika kufika mahakamani, ambapo baada ya kujaza taarifa zinazohitajika, mfumo humwelekeza namna ya kulipia gharama zinazohitajika kulingana na aina ya shauri, kupitia namba maalum ya malipo (Control Number).

Amesema kwa mwananchi ambaye hana akaunti katika mfumo huo, anaweza kupata usaidizi wa Wakili yoyote wa Mahakama, kwa kuwa Mawakili wote wanafahamu hatua zinazotakiwa kufuatwa.

Kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma za wakili, Mariki amesema Mahakama Kuu imeweka kioski maalum chenye wataalamu wa TEHAMA, ambao hutoa usaidizi katika hatua mbalimbali za kufungua shauri kupitia mfumo huo.

Mheshimiwa Mariki amebainisha kuwa, baada ya taarifa zote zinazohitajika kujazwa kwenye mfumo kukamilika, mwananchi hupokea taarifa mbalimbali kupitia mfumo huo, ikiwemo taarifa ya kupokelewa kwa shauri lake, jina la Jaji aliyepangiwa kulisikiliza, tarehe ya kusikilizwa na hatua nyingine zinazoendelea. Mfumo pia humwezesha mwananchi kufuatilia mwenendo mzima wa kesi yake.

Ameeleza matumizi ya mfumo huo yameleta faida mbalimbali, ikiwemo kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakitokana na makosa ya kibinadamu, kupunguza gharama za kufuatilia mashauri kwa wananchi na kupunguza mazingira ya rushwa kutokana na kupungua kwa mawasiliano ya ana kwa ana.

Amesema pia mfumo huo umepunguza uzembe kwa baadhi ya watendaji wa Mahakama wasio waaminifu, ikiwemo ucheleweshaji wa mashauri bila sababu za msingi, kwa kuwa viongozi wengine wa Mahakama wanaweza kufuatilia mwenendo wa kesi kupitia mfumo huo.

Kwa upande wa mashauri ya rufaa kutoka Mahakama za chini, Mheshimiwa Mariki amesema mfumo huo umeondoa ucheleweshaji uliokuwa ukitokana na kusubiri majalada kutoka Mahakama hizo, kwa kuwa kwa sasa majalada yote ikiwemo hukumu zilizotolewa vinapatikana kwenye mfumo.

Aidha, amesema mfumo huo unamwezesha wakili kusimamia shauri bila kulazimika kufika mahakamani kwa kila hatua, jambo ambalo limewasaidia Mawakili wenye mashauri mengi katika maeneo mbalimbali kuepuka changamoto ya mwingiliano wa tarehe za kesi.

Kwa upande wa mashahidi, amesema mfumo huo pia unawawezesha kutoa ushahidi kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika mahakamani, isipokuwa kwa ushahidi unaohitaji uthibitisho wa nyaraka ambao shahidi mwenye nyaraka anatakiwa kufika mahakamani.

Aidha, kwa baadhi ya watuhumiwa wa makosa ya jinai, wakiwemo wagonjwa na waliopo gerezani, mfumo huo unawawezesha kusikilizwa kwa njia ya mtandao kwa kibali maalum cha Mahakama, bila kulazimika kufika mahakamani.

Hata hivyo, Mheshimiwa Mariki ameitaja changamoto iliyopo katika matumizi ya mfumo huo ni ugeni wa baadhi ya wananchi katika namna ya kuutumia, udhaifu wa mtandao wa intaneti katika baadhi ya maeneo na hasa ya vijijini, pamoja na baadhi ya watu kutokuwa na imani kwamba wanaweza kupata huduma na kusikilizwa bila kufika mahakamani.

Amezieleza changamoto hizo kuwa ni ndogo na siyo kikwazo katika uendeshaji wa mashauri , kwa kuwa nyingi hutatuliwa kwa muda mfupi kupitia wataalam wa Mahakama.

Post a Comment

0 Comments