
![]() |
| Mh. Azzah Hilal Hamad, Mbunge wa Jimbo la Itwangi |
Ninamfahamu
Azzah kupitia maoni ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga niliyofika
wakati wa kutekeleza majukumu yangu ya uandishi wa Habari. Katika maeneo yote
niliyopita, nilikutana na wananchi waliomzungumzia kwa mtazamo chanya na
kueleza namna walivyovutiwa na uongozi wake.
Azzah ni Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Itwangi, lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga.
Katika
kipindi hicho, alijijengea jina, hususan miongoni mwa wanawake na wananchi wa
kawaida, kutokana na mtindo wake wa uongozi uliotanguliza ukaribu na jamii,
usikivu na ushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Azzah
anaonekana kuwa kiongozi mpole, asiye na majivuno na anayejali changamoto za
wengine. Hii ni sifa muhimu katika uongozi, hasa katika kipindi ambacho baadhi
ya wanasiasa wanapopata nyadhifa za uongozi husahau umuhimu wa kuwa karibu na
wananchi waliowaamini na kuwapa dhamana ya kuwaongoza.
Kiongozi
hapaswi kubadilika na kujitenga na wananchi baada ya kupata madaraka. Badala
yake, nafasi ya uongozi inapaswa kuwa daraja la kuimarisha mawasiliano kati
yake na wananchi, ili changamoto zao zisikilizwe na kufanyiwa kazi kwa wakati.
Katika
kipindi chake cha kuwa Mbunge wa Viti Maalum, Azzah alishiriki kwa ukaribu
katika masuala mbalimbali ya kijamii. Inasemekana
kwamba, hata ujenzi wa kituo cha afya Tinde ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa
wakazi wa Tinde na maeneo jirani ulikamilika kwa haraka kutokana na ushawishi
wake na akahakikisha kinakuwa na gari la wagonjwa.
Pamoja na
kuchangia kwake miradi mingi ya maendeleo na kijamii, vilevile alisaidia
vikundi mbalimbali vya wanawake, hatua iliyomwezesha kuimarisha uhusiano wake
na kundi hilo na jamii kwa ujumla.
Safari ya
kisiasa ya Azzah haikukosa vikwazo. Baada ya kumaliza kipindi chake cha Ubunge
wa Viti Maalum mwaka 2020, aligombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Solwa, ambako
alishindwa katika kura za maoni za CCM.
Baadaye, Mei
29, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
alimteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, lakini uteuzi huo ulifutwa
baadaye kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
Pamoja na
changamoto hizo, Azzah alibaki kuwa mtulivu. Aliendelea na safari yake ya
kisiasa katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo alijitokeza
tena kutafuta nafasi ya kugombea ubunge kupitia chama chake.
Kabla ya
uchaguzi huo, Jimbo la Solwa liligawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Itwangi.
Hatua hiyo ilizua maoni mbalimbali miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wakiwemo
wananchi wa kawaida, ingawa majibu ya jambo hilo yalibaki mikononi mwa Tume
huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya kufanya
hivyo.
Azzah
alijitosa kuomba ridhaa kwenye chama
chake cha CCM kuteuliwa kuwa mgombea Ubunge
wa Jimbo jipya la Itwangi, ambapo katika kura ya maoni, aliibuka mshindi dhidi
ya wenzake waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ndani ya chama akiwemo Katibu wa
Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa
wa Shinyanga ni Ndugu Richard Masele.
Katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Azzah aliibuka mshindi na kuwa Mbunge wa kwanza wa
Jimbo la Itwangi. Ushindi huo uliashiria hatua nyingine katika safari yake ya
kisiasa.
Mwanzoni,
nilidhani kwamba Azzah aliweza kuwa karibu na wananchi kwa kiwango hicho kwa
sababu alikuwa Mbunge wa Viti Maalum na hakuwa na majukumu mengi kama
waliyonayo wabunge wa majimbo.
Hata hivyo,
baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Itwangi, nimeendelea kuona umuhimu
wa mtindo wake wa uongozi unaotanguliza ukaribu na wananchi.
Jambo
jingine linalomtofautisha ni namna anavyotumia muda wake kuwa karibu na
wananchi. Licha ya uwepo wa shughuli za kiuongozi zinazoweza kumpeleka katika
miji mikubwa kama Dar es Salaam na Dodoma, amekuwa akitumia muda mwingi katika
eneo analoliongoza, huku makazi yake kwa muda mwingi yakiwa katika Kijiji cha
Jomu, Tinde.
Ukaribu huo
unampa fursa ya kufahamu hali halisi ya maisha ya wananchi, kusikiliza kero zao
na kutafuta namna ya kuzitatua kupitia nafasi yake ya uongozi, tofauti na
baadhi ya viongozi ambao baada ya kuchaguliwa hujitenga na wapiga kura wao kwa
kuhamishia makazi yao kwenye miji mikubwa kama Dar es salaam na kuja kwenye
Jimbo lake tu kuchungulia kunapokuwa na sababu fulani au ziara za viongozi
wakubwa.
Ni kweli
kwamba changamoto zinazowakabili wananchi ni nyingi na si zote zinazoweza kutatuliwa
kwa wakati mmoja. Hata hivyo, wananchi hupata faraja wanapokuwa na kiongozi
anayewasikiliza, kuwapa moyo na kuonyesha utayari wa kushirikiana nao kutafuta
ufumbuzi wa matatizo yao.
Azzah
amekuwa akijitokeza mara kwa mara katika shughuli za maendeleo, kusikiliza kero
za wananchi na kutafuta namna ya kuzitatua. Huu ndio uongozi unaohitajika
katika jamii, kwa sababu wananchi wanahitaji viongozi wanaoweza kufikiwa na kusikiliza
mahitaji yao bila kuwafanya wajisikie kuwa ni kero.
Baadhi ya
wananchi wa Jimbo la Itwangi wamebainisha kuwa, tangu achaguliwe kuliongoza
jimbo hilo, Mbunge huyo amefanya mambo mengi ambayo ni pamoja na kusukuma mbele
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya
barabara hasa katika maeneo ya vijijini, ujenzi wa Zahanati, Miradi ya maji na
kuwezesha vikundi mbalimbali vya wananchi wake.
Wamemwelezea
mbunge huyo kuwa, muda wote wanapohitaji kumuona wanaweza kumfikia bila vikwazo
na pale anapotoka Bungeni huwafuata kwenye maeneo yao ikiwemo vijijini, ambako
hushirikiana nao mambo mbalimbali pamoja na kusikiliza kero zao kupitia mikutano
ya hadhara.
Wananchi na
baadhi ya Viongozi wenzake wamebainisha kuwa, Mbunge huyo amekuwa akiwashirikisha kwa karibu
hata kuhusu matumizi ya fedha za mfuko
wa Jimbo na kuzigawa kadiri ya mahitaji yao kwa kutoa kipaumbele kwenye maeneo
yenye uhitaji zaidi.
Jambo
jingine linalostahili kuangaliwa ni namna anavyowasiliana na watu wenye
mitazamo tofauti. Katika siasa, kutofautiana kwa mawazo ni jambo la kawaida,
lakini tofauti hizo hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, matusi, ubaguzi au
kudharauliana.
Huwezi
kumsikia Azzah kwenye mikutano yake
akitumia jukwaa kuwasema vibaya,
kuwabeza, kuwakejeli wala kutumia lugha za kibaguzi dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa,
hali ambayo imemwongezea ushawishi kwa kundi kubwa la watu bila kujali tofauti
zao za kiitikadi na chama alichotoka.
Hata pale
anapokutana na maoni ambayo hakubaliani nayo, ana uwezo wa kusikiliza na kujibu
kwa utulivu ambayo ni sifa muhimu kwa kiongozi. Hii haimaanishi kwamba kiongozi
hapaswi kusimamia msimamo wake, bali anapaswa kufanya hivyo kwa hekima, busara,
kujali hisia za wengine na kuzingatia maslahi ya umma.
Mtindo wa
siasa anazozifanya Mbunge huyo umemwezesha kupunguza idadi ya maadui na watu
wanaompinga ndani na nje ya chama chake, hivyo kutolazimika kutumia nguvu
nyingi kutimiza jambo lake.
Ni jambo la
nadra sana hata kwa viongozi wa upinzani kukuta wanamshambulia Azzah kwenye
majukwaa kama wanavyoshambuliwa viongozi wengine.
Kwa mtazamo
wangu, Azzah ameonyesha umuhimu wa kujenga siasa zinazolenga maendeleo na
utatuzi wa changamoto za wananchi badala ya kutumia muda mwingi kushambulia
wapinzani. Mtindo huu unasaidia kujenga mazingira ambayo watu wenye mitazamo
tofauti wanaweza kuendelea kuishi pamoja na kushirikiana katika masuala ya
maendeleo.
Ni kwa
sababu hizo ninawaomba viongozi wote wanaopata dhamana kupitia uchaguzi
kuutazama mfano huu na kujifunza umuhimu wa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza
maoni yao na kushughulikia kero zao bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au
kiuchumi.
Viongozi
wanapaswa pia kuelewa kwamba si kila mwananchi anayekutana nao anahitaji kupewa
fedha. Wakati mwingine, mtu anayepitia changamoto anahitaji kusikilizwa,
kufarijiwa, kupewa mwongozo au kusaidiwa kupata huduma inayomfaa.
Ni kweli
kwamba uwezo wa kifedha wa viongozi unatofautiana, na si kila changamoto
inaweza kutatuliwa kwa fedha zao binafsi. Hata hivyo, kila kiongozi ana wajibu
wa kutumia nafasi aliyonayo kuunganisha wananchi na fursa, kusimamia
upatikanaji wa huduma na kuhakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wale
waliokusudiwa.
Kwa msingi
huo, ukaribu wa Azzah na wananchi unapaswa kuwa somo kwa viongozi wengine
kwamba, uongozi si suala la kushika cheo pekee, bali ni dhamana inayohitaji
unyenyekevu, usikivu, uwajibikaji na utayari wa kuwatumikia watu.
Mwisho wa siku, wananchi hawatakumbuka tu vyeo vya viongozi wao, bali watakumbuka namna walivyowatendea, walivyowasikiliza na hatua walizochukua kuboresha maisha yao. Huo ndio msingi wa uongozi unaostahili kuigwa.

0 Comments