MADIWANI KAHAMA WATAKA KUUNDWA KWA MKOA MAALUMU WA TANESCO KUBORESHA USIMAMIZI WA HUDUMA ZA UMEME

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wameiomba Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuanzisha mkoa maalumu wa TANESCO wa Kahama, ili kurahisisha utatuzi wa changamoto za umeme pamoja na kuboresha usimamizi na utoaji wa huduma.

Hoja hiyo imetolewa na Diwani wa Kata ya Nyahanga, Josephine Kilimba, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kilichofanyika leo tarehe 25, Novemba, 2026, katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.

Diwani wa Kata ya Nyahanga, Josephine Kilimba

Akiwasilisha hoja hiyo, Kilimba amesema Manispaa ya Kahama ina shughuli nyingi za kiuchumi zinazotegemea nishati ya umeme, ambazo zinachangia kwa kiwango kikubwa mapato ya halmashauri na Taifa kwa ujumla.

Amesema hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara inaathiri shughuli hizo na kudhoofisha kasi ya maendeleo, hivyo kuanzishwa kwa mkoa maalumu wa TANESCO wa Kahama kutaliongezea nguvu shirika katika eneo hilo lenye uwekezaji mkubwa, hatua ambayo itasaidia kurahisisha usimamizi na utoaji wa huduma za umeme, pamoja na kuwezesha changamoto zinazojitokeza kushughulikiwa kwa wakati.

Aidha, amebainisha kuwa, hatua hiyo itawezesha Wilaya nzima ya Kahama yenye Halmashauri tatu za manispaa ya Kahama, Ushetu na Msalala kuwa na bajeti  maalumu kwa ajili ya kushughulikia changamoto za umeme, badala ya kuendelea kutegemea mambo mengi kutoka makao makuu ya mkoa, yaliyoko mjini Shinyanga.

Hoja hiyo imeungwa mkono na madiwani wote, huku Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, akiahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na uongozi wa TANESCO.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu

Katika hatua nyingine, madiwani, mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Adonias Nyamjulirwa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Kahama, Joachim Edward Simbila, wamewapongeza watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama wakiongozwa na Mkurugenzi Masudi Kibetu, kwa juhudi za ukusanyaji wa mapato wanazozifanya.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Adonias Nyamjulirwa

Wamesema juhudi hizo zimechangia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo katika kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2026/2027, Manispaa ya Kahama imekuwa kinara kwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.1 kwa vikundi 96.

Wamewataka watendaji wa halmashauri kuendelea kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kahama, Mataluma Kaniki, amewataka madiwani kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao, pamoja na kusimamia matumizi sahihi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi hiyo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama, Mataluma Kaniki

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, aliwashuri madiwani kuweka utaratibu  maalum kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yao, ili waweze kufahamu changamoto zinazowakabili na kuona namna ya kuzitafutia ufumbuzi kupitia nafasi waliyonayo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum

Kikao hicho pia kilipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo kutoka kata mbalimbali, kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, iliyoanza kipindi cha Julai hadi Septemba 2026.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Kahama, Joachim Edward Simbila

 

Post a Comment

0 Comments