MAAGIZO NA MAMBO AMBAYO WAZIRI MKUU NCHEMBA AMEYAPIGA MARUFUKU KWENYE SEKTA YA AFYA

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amepiga marufuku hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya kuwachangisha fedha kwa ajili ya kununua mafuta ya gari ndugu wa wagonjwa wanaopewa rufaa, akionya kuwa watendaji watakaokiuka maelekezo hayo watachukuliwa hatua.

Dkt. Nchemba ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake mkoani Shinyanga, ambapo ameyakazia zaidi wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Shinyanga kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika leo tarehe 9, Novemba, 2026, katika uwanja wa JASCO.

Amesema Serikali inatenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa magari ya wagonjwa na kuajiri madereva, hivyo hakuna sababu ya ndugu wa wagonjwa kuchangishwa fedha ya mafuta pale wanapohitaji huduma ya usafiri wa dharura baada ya kupewa rufaa na kwamba, jambo hilo limekuwa likisababisha ucheleweshaji wa huduma na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Amewataka viongozi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati kuhakikisha magari hayo yanakuwa na mafuta wakati wote, ili yaweze kutoa huduma pindi dharura inapojitokeza.

Mheshimiwa Nchemba pia ameendelea kupiga marufuku utaratibu wa kuwasubirisha mapokezi wajawazito na wagonjwa wa dharura na badala yake ameelekeza wahudumiwe kwanza na baadaye taratibu nyingine zifuate ili kuokoa maisha.

Katika hatua nyingine, ameelekeza kufuatiliwa kwa kina kwa changamoto ya upatikanaji wa dawa katika hospitali za umma, baada ya kubainisha kuwa kuna malalamiko ya wagonjwa kuelekezwa kununua dawa katika maduka ya nje, hata zile za kawaida, licha ya taarifa za Wizara ya Afya kuonesha kuwa utoshelevu wa dawa umefikia zaidi ya asilimia 90.

Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, hivyo inahitaji ufuatiliaji wa kina, ili kubaini sababu za wagonjwa kukosa dawa katika vituo vya umma na kuwachukulia hatua watendaji watakaobainika kuhujumu juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya. 

Amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na watendaji walioko chini yake kusimamia utoaji wa dawa zinazoletwa na Serikali na kuhakikisha wanaagiza kulingana na mahitaji halisi ya wananchi, kwa kuzingatia dawa zinazohitajika zaidi katika maeneo yao.

Aidha, Dkt. Nchemba amewataka watendaji wa sekta ya afya kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wazingatie miongozo na maelekezo ya Serikali, ikiwemo kuwahudumia wagonjwa kwa wakati bila kuchelewesha huduma. 

Waziri Mkuu ameonya dhidi ya watumishi wanaobeza na kupuuza maelekezo ya Serikali kwa madai kuwa ni ya kisiasa, akisisitiza kuwa, maagizo yote yanayotolewa yanapaswa kupewa uzito unaostahili na kwamba, watakaobainika kwenda kinyume chake watachukuliwa hatua.

Amesema Serikali haitakuwa tayari kuwafumbia macho watumishi wazembe wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo ya kazi na maelekezo yanayotolewa na Serikali, ambapo amewataka waajiri kuwachukulia hatua ikiwemo kuwaondoa  kazini badala ya kuwahamishia vituo vingine.

Nchemba amewashauri  wananchi kutokaa kimya pale wanapotendewa vibaya na watumishi wa umma na badala yake wachukue utambulisho wao na kutoa taarifa kwa mamlaka za juu ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao.

Post a Comment

0 Comments