Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba, kesho
Jumapili tarehe 8, Novemba, 2026,
ataanza ziara yake ya siku nne mkoani
Shinyanga, akitokea mkoani Simiyu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, Waziri Mkuu Nchemba ataanzia ziara yake katika wilaya ya Kishapu, ambapo atazungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa SHIRECU.
Keshokutwa Jumatatu tarehe 9, Novemba, 2026, Mheshimiwa Nchemba, atafanya ziara yake katika Jimbo la Solwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Iselamagazi na baadaye atarejea katika Manispaa ya Shinyanga na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara, utakaofanyika katika uwanja wa JASCO uliopo Kata ya Ngokolo.
Jumanne tarehe 10, Novemba, 2026, Waziri Mkuu Nchemba atatembelea Jimbo la Itwangi katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambapo atazungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Usanda Kata ya Usanda na baadaye ataelekea katika Manispaa ya Kahama na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara, utakaofanyika katika Kata ya Majengo mjini Kahama.
Jumatano tarehe 11, Novemba, 2026, Waziri Mkuu Nchemba ataelekea katika Halmashauri ya Ushetu na kuzungumza na wananchi katika uwanja wa Nyamilangano uliopo katika Kata ya Nyamilangano, ambapo baadaye ataelekea katika Halmashauri ya Msalala na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Kata ya Segese.
Kupitia ziara hiyo, Waziri Mkuu Nchemba pia atatembelea miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo mradi wa taasisi ya elimu ya ushirika na biashara uliopo Kizumbi katika Manispaa ya Shinyanga, mradi wa jengo la Mama na mtoto lililopo katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, mradi wa shule ya mafunzo ya amali iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu na atakagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Lami kutoka Kahama kwenda Bulyanhulu, unaotekelezwa katika Halmashauri ya Msalala.
Mheshimiwa Mboni amewaomba wananchi wa mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo waziri Mkuu Nchemba, atafika.

0 Comments