KONGAMANO LA MISA TAN WADAU 2026; TAASISI ZA UMMA ZAHIMIZWA KUSHIRIKIANA NA WANAHABARI

 

Mkuu wa mkoa wa Mwanza CP Salum Hamduni, amezitaka taasisi za umma kuimarisha mazingira ya kuwawezesha wanahabari kupata taarifa sahihi,  ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya mipango ya Serikali na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hamduni ametoa rai hiyo kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Daniel Machunda, katika ufunguzi wa Kongamano maalum la Taasisi ya vyombo  vya Habari kusini mwa Afrika ,Tawi la Tanzania (MISA TAN) na taasisi za umma na binafsi, lililofanyika katika ukumbi wa BoT, Jijini Mwanza.

Hamduni ameieleza hatua ya taasisi za umma kushirikiana na wanahabari  inatoa fursa muhimu ya  kueleza kwa uwazi majukumu yao na huduma wanazozitoa, ili kujenga jamii yenye uelewa na kwamba, utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi inahitaji ushirikiano na wadau wakiwemo waandishi wa Habari.

Amezihimiza taasisi zote za umma kuweka mifumo madhubuti ya mawasiliano na vyombo vya Habari na kutambua umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati, hatua ambayo itawawezesha waandishi wa Habari kupata ufafanuzi wa masuala yenye maslahi kwa umma.

Hamduni amewaomba waandishi wa Habari kuendelea kujenga mahusiano ya kitaaluma na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za umma, na kuhakikisha wanaongeza kasi ya kutangaza shughuli za maendeleo na fursa za kiuchumi zilizopo katika mikoa yao na taifa kwa ujumla, huku wakihakikisha wanazingatia misingi ya kitaaluma ikiwemo kufanya utafiti wa kina ambao utawawezesha kutoa taarifa sahihi na zenye maslahi kwa taifa.

Ameipongeza MISA TAN kwa kuandaa kongamano hilo huku akilitaja kuwa  litaimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya waandishi wa Habari na taasisi za umma na kwamba, taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ushirikiano na wadau ambao ni nguzo kubwa katika kuchochea uchumi wa  nchi.

Aidha, amezipongeza taasisi za umma zilizodhamini na kufanikisha maandalizi ya kongamano hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MISA TAN, Bw. Edwin Soko, ameahidi taasisi hiyo kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau ikiwemo taasisi za umma huku akibanisha kuwa, vyombo vya Habari vina nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo.

Mwenyekiti wa MISA TAN Bw. Edwin Soko

Soko amebainisha kwamba, tasisi hiyo itahakikisha wanachama wake wanabeba jukumu la kuandaa vipindi na kuchapisha taarifa kwa weledi na kwa kuzingatia maadili, wakiongozwa na moyo wa uzalendo na kutanguliza mbele maslahi ya umma.

Soko amewashukuru wadau wote waliodhamini Kongamano hilo ambao ni Benki kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mwanza, Mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma (PSSSF), Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Idara ya uhamiaji, Shirika la Meli Tanzania (TASHICO) Mamlaka ya usimamizi wa bima Tanzania (TIRA), Mamlaka ya hifadhi za Taifa (TANAPA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Wadhamini wengine ni Kampuni binafsi zinazozalisha vinywaji vikali na baridi za TBL na SBC inayozalisha na kusambaza vinywaji baridi vya chapa ya PEPSI

Nao wadau waliodhamini Kongamano hilo ambao baadhi yao wamepata nafasi ya kutoa elimu kwa waandishi wa Habari kuhusu huduma wanazozitoa, wameahidi kuendelea kushirikiana na MISA TAN, huku wakibanisha kuwa, wanafanya hivyo kwa kuwa wanatambua mchango mkubwa wa wanahabari katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yenye ustawi kwa wananchi.

Kongamano hilo lililopewa jina la “MISA TAN WADAU 2026” limewakutanisha waandishi wa Habari zaidi ya 60 wakiwemo Wahariri kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na Kanda ya Magharibi, likiwa na lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa kisekta kupitia uandishi wa Habari.

Post a Comment

0 Comments