Kwanza,
ninalipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kazi kubwa linayofanya ya kulinda raia
na mali zao. Jeshi hili lina nafasi muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama
kwa kuzuia uhalifu kabla haujatokea na kukabiliana nao pale unapotokea, hata
katika mazingira hatarishi kwa maisha ya askari wake.
Nimewahi kujiuliza, kama kusingekuwa na Jeshi la Polisi, hali ingekuwaje? Bila shaka, pasipo chombo hiki cha kusimamia sheria na usalama, baadhi ya watu wangeweza kutumia nguvu zao kuwaumiza wengine, kunyang'anya mali zao au kuwafanyia vitendo vingine vya uhalifu bila hofu ya kuwajibishwa.
Uwepo wa Jeshi la Polisi umesaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti vitendo hivyo, huku hofu ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwazuia baadhi ya watu wenye nia ya kutenda uhalifu.
Pili, ninalipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kuanzisha kampeni ya Ongea na Kamanda wa Polisi, inayolenga kuwakutanisha wananchi na makamanda wa polisi katika mikoa yao, ili kusikiliza na kutatua kero zinazohusu masuala ya ulinzi na usalama.
Zaidi sana, nimpongeze Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, kwa kuitendea haki kampeni hiyo, kwa sababu ameitekeleza kwa kufika chini kabisa kwa wananchi mpaka vijijini na kuzungumza nao moja kwa moja.
Kwa kawaida, makamanda wa polisi huonekana katika maeneo ya vijijini zaidi kunapokuwa na matukio makubwa ya uhalifu au ziara za viongozi wa Serikali. Hivyo, kuwafikia wananchi katika mazingira yao ya kawaida ni hatua muhimu inayoweza kujenga uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na jamii.
Hatua hiyo itasaidia wananchi kuliona Jeshi la Polisi kama mdau muhimu wa usalama wao, badala ya kuwa chombo wanachokiogopa au kukiona kama adui.
Vilevile, inaweza
kuimarisha ushirikiano katika kupambana na uhalifu, hususan kwa wananchi kutoa
taarifa mapema kuhusu viashiria vya uhalifu katika maeneo yao.
Hata hivyo, ninasisitiza kuwa, makamanda wa Polisi wanapaswa kuyasikiliza kwa makini malalamiko ya wananchi na kuyafanyia kazi.
Kampeni hii haitakuwa na manufaa yanayotarajiwa, ikiwa itafanyika kwa mazoea au kama njia ya kutimiza wajibu bila kuhakikisha kuwa, kero zinazowasilishwa na wananchi zinapatiwa ufumbuzi.
Kupitia kampeni hiyo, wananchi wamekuwa wakieleza kero mbalimbali na kutoa mapendekezo ya kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi, ili huduma zake ziendelee kuwa na manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Miongoni mwa kero zinazojitokeza mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ni changamoto za upatikanaji wa dhamana katika vituo vya Polisi, hasa kwa watuhumiwa wa makosa yanayodhaminika.
Malalamiko hayo yanapojirudiarudia katika maeneo tofauti, yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito na mamlaka husika.
Nimewahi kuzungumza na baadhi ya wananchi kwa siku kadhaa ili
kupata ufafanuzi kuhusu suala hili.
Walinieleza kuwa, katika baadhi ya vituo vya Polisi, ndugu zao wanapokamatwa, hukumbana na usumbufu na ucheleweshaji wa kupata dhamana, hata katika mazingira ambayo wanaamini makosa yanayowakabili yanadhaminika.
Iwapo hali hii inatokea kutokana na uzembe au ukiukwaji wa taratibu, inaweza kufungua mwanya wa vitendo vya rushwa, ambapo baadhi ya maafisa wa Polisi wasio waaminifu wanaweza kutumia nafasi zao kudai fedha kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa ili kuwawezesha kupata dhamana.
Nakumbuka tukio la miaka kadhaa iliyopita katika kituo kimoja cha Polisi, ambapo mkuu wa kituo (OCS) aliamua kuwahoji watuhumiwa mmoja mmoja waliokuwa wakishikiliwa mahabusu kuhusu makosa yaliyokuwa yanawakabili.
Katika uchunguzi huo, alibaini kuwa baadhi yao walikuwa na sifa za kupewa dhamana lakini hawakuwa wamepatiwa huduma hiyo. Kiongozi huyo alihoji kwa walioko chini yake sababu za kucheleweshwa kwa dhamana na kuagiza watuhumiwa wote waliokidhi vigezo vya kisheria wapelekwe Ofisini kwake ili wapewe dhamana mara moja.
Tukio hilo linaonesha umuhimu wa usimamizi wa karibu wa viongozi wa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha kuwa, watuhumiwa wanapatiwa haki zao kwa mujibu wa sheria.
Ingawa
sheria zinaweka utaratibu wa dhamana kwa makosa yanayodhaminika, malalamiko ya
wananchi yanaashiria kuwa, bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili
kuhakikisha taratibu hizo zinafuatwa ipasavyo.
Ni muhimu kusisitiza kuwa, dhamana si upendeleo, bali ni utaratibu wa kisheria unaopaswa kusimamiwa kwa haki na bila ubaguzi.
Ni muhimu kusisitiza kuwa, dhamana si upendeleo, bali ni utaratibu wa kisheria unaopaswa kusimamiwa kwa haki na bila ubaguzi.
Hata hivyo, utoaji wake hutegemea masharti ya sheria na mazingira ya kila kesi. Kwa hiyo, pale ambapo mtuhumiwa anastahili dhamana, taratibu zinazohusika zinapaswa kufuatwa bila ucheleweshaji usio na sababu za msingi.
Ili kupunguza malalamiko haya na kuimarisha imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi, ninapendekeza hatua kadhaa zichukuliwe.
Kwanza, taarifa kuhusu dhamana ziwekwe wazi katika vituo vyote vya Polisi. Maandishi yanayoonekana na kusomeka kwa urahisi yabandikwe katika maeneo ya wazi, yakieleza taratibu za kuomba dhamana, vigezo vinavyohusika na hatua za kufuata endapo mtuhumiwa atakabiliwa na changamoto katika kupata haki hiyo.
Taarifa hizo pia zieleze namna ya
kuwasilisha malalamiko pale kunapokuwa na madai ya ukiukwaji wa taratibu za
kisheria.
Pia, utasaidia kujenga mahusiano bora kati ya polisi na jamii, jambo ambalo ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kupambana na uhalifu.
Kwa msingi huo, ninatoa wito kwa uongozi wa Jeshi la Polisi kulichunguza kwa kina suala la dhamana katika vituo vyake na kuhakikisha kuwa, kila mtuhumiwa anayetimiza masharti ya kisheria anapatiwa haki yake kwa wakati. Vilevile, wananchi wanapaswa kuendelea kutumia njia rasmi kuwasilisha malalamiko yao pale wanapoona taratibu za kisheria hazifuatwi.
Jeshi la Polisi linapolinda haki za wananchi na kusimamia sheria kwa usawa, linajenga imani ya umma na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika kulinda usalama wa kila mmoja wetu.

0 Comments