WANANCHI TOENI TAARIFA KWA MAMLAKA KUHUSU MAENEO HATARISHI

 

Kwa sasa, viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali nchini, wamekuwa wakisisitiza mikakati na hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Jambo hilo ni zuri na linaonyesha umuhimu ambao Serikali imeuweka katika kuwalinda wananchi, hasa baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kunyesha kwa mvua za juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini, hali ambayo inaweza kusababisha mafuriko na madhara mengine.

Viongozi wa juu wa Serikali, akiwemo Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, tayari wametoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi za chini kuhakikisha wananchi wanaandaliwa na kuchukua hatua za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Serikali pia imetenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na madhara hayo kabla, wakati na baada ya kutokea.

Hata hivyo, pamoja na maandalizi hayo, kuna jambo lingine muhimu linalopaswa kupewa uzito: ushirikishwaji wa wananchi katika kubaini maeneo yanayoweza kuwa hatarishi.

Wananchi ndio wanaoyafahamu vizuri mazingira wanamoishi.

Wanaweza kubaini mapema maeneo ambayo maji yamekuwa yakituama, njia za asili za maji zilizozibwa au kuharibiwa, pamoja na maeneo ambayo yamekuwa hatarishi kutokana na kufunguliwa kwa barabara au shughuli nyingine bila kuwekwa mifereji na njia sahihi za kupitisha maji.

Kwa hiyo, natoa rai kwa wananchi kutokaa kimya. Wanapaswa kutoa taarifa kwa viongozi na mamlaka husika kuhusu maeneo hayo ili hatua za kuyarekebisha zichukuliwe kabla mvua kubwa hazijaanza kunyesha.

Hatua hizo zinaweza kujumuisha kusafisha na kutengeneza mifereji, kuweka kalavati, kurekebisha njia za maji na kuhakikisha maji yanaelekezwa katika maeneo salama badala ya kusambaa kwenye makazi ya wananchi.

Wakati huo huo, mamlaka katika ngazi mbalimbali zinapaswa kuweka utaratibu mzuri wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi, kuzifanyia kazi na kutembelea maeneo yanayotajwa kuwa hatarishi badala ya kuishia tu kwenye kufanya usafi na kuokota karatasi kwenye maeneo ya mijini. 

Hii itasaidia kutambua changamoto hizo mapema na kuchukua hatua stahiki kabla hazijageuka kuwa majanga.

Tusisubiri madhara yatokee ndipo tuanze kutafuta suluhisho. Kinga ni bora kuliko tiba. Ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka ni muhimu katika kuhakikisha maeneo hatarishi yanabainishwa na kushughulikiwa mapema.

Wananchi, huu ni wakati wa kutoa taarifa. Mkitambua eneo hatarishi katika maeneo yenu, lisemeni ili hatua zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.

Mkitoa taarifa halafu mamlaka zisichukue hatua mtakuwa na cha kusema:  “Tulitoa taarifa lakini hatua hazikuchukuliwa, ndiyo maana yametokea haya” hapo mnaweza kuwa na nguvu hata za kuelekeza lawama kwa mamlaka ambayo haikujali baada ya kuipa taarifa.

Post a Comment

0 Comments