MAADHIMISHO YA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA: SHINYANGA KUELIMISHA UMMA KUHUSU UMUHIMU WA TAKWIMU

 


Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa nchini Tanzania itakayoungana na maeneo mengine nchini na barani Afrika kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika, inayoadhimishwa Novemba 18 kila mwaka, kwa lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya takwimu katika kupanga, kufanya maamuzi na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Meneja Takwimu Mkoa wa Shinyanga, Bw. Eliud Weston Kamendu, maadhimisho hayo ambayo kitaifa yatafanyika jijini Dodoma, katika mkoa wa Shinyanga yatafanyika kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya takwimu, ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa takwimu katika kuwezesha Serikali na wadau mbalimbali kupanga na kutekeleza mipango inayokidhi mahitaji ya jamii.

Amesema elimu hiyo itatolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia vyombo vya Habari, wakijielekeza zaidi kwenye kaulimbiu ya mwaka huu inayojikita katika kuweka mifumo rasmi ya takwimu za maji na usafi wa mazingira, kwa ajili ya maendeleo endelevu yanayostahimili hali ya mabadiliko ya tabianchi.
Meneja Takwimu Mkoa wa Shinyanga, Bw. Eliud Weston Kamendu

Kamendu ameitaja kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema kuwa: “Kuweka mifumo rasmi ya takwimu za maji na usafi wa mazingira kwa maendeleo endelevu yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi.”

Mkoa wa Shinyanga, ambao una wilaya tatu za Shinyanga, Kahama na Kishapu pamoja na Halmashauri sita, ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (vijijini), Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kahama, Kishapu, Msalala na Ushetu, una jumla ya watu 2,241,299 kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Hata hivyo, kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya watu ya mwaka 2026, mkoa huo unakadiriwa kuwa na jumla ya watu 2,558,483.

Aidha, Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,  zinaitaja Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (vijijini) kuwa inaongoza kwa kuwa  na watu 468,611, sawa na asilimia 20.9 ya wakazi wote wa mkoa huo, ambapo idadi hiyo inakadiriwa kufikia watu 533,462  kwa, mwaka 2026.

Manispaa ya Kahama inafuatia kwa kuwa na watu 453,654, sawa na asilimia 20.3 ya wakazi wote wa mkoa, huku idadi hiyo ikikadiriwa kufikia watu 518,750, mwaka 2026.

Halmashauri ya Ushetu ina watu 390,593, sawa na asilimia 17.4 ya wakazi wote, na kwa mwaka 2026 inakadiriwa kuwa na watu 445,935.

Kwa upande wa Halmashauri ya Msalala ina jumla ya watu 378,214, sawa na asilimia 16.9 ya wakazi wote wa mkoa, huku idadi hiyo ikikadiriwa kufikia watu 428,575, mwaka 2026.

Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ina jumla ya watu 335,483, sawa na asilimia 15.0 ya wakazi wote wa mkoa ambapo kwa mwaka 2026, inakadiriwa kuwa na watu 384,882.

Kwa upande wa Manispaa ya Shinyanga ina jumla ya watu 214,744, sawa na asilimia 9.6 ya wakazi wote wa mkoa, huku idadi hiyo ikikadiriwa kufikia watu 246,879 , kwa mwaka huu 2026.

Post a Comment

0 Comments