Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekuwa akitoa maagizo mbalimbali kwa niaba ya Serikali, kupitia ziara anazofanya katika maeneo tofauti nchini.
Maagizo mengi yanatokana na malalamiko na kero zinazowasilishwa na wananchi kupitia mikutano ya hadhara, ambayo amekuwa akiitumia kama fursa ya kusikiliza changamoto zao na kuelekeza namna ya kuzitatua.
![]() |
| Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba |
Nimpongeze
kwa hatua hiyo, kwani wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
zinazohitaji ufumbuzi wa Serikali, lakini wakati mwingine hukosa fursa au
mahali sahihi pa kuziwasilisha ili zipatiwe ufumbuzi.
Zaidi ya
hilo, ninampongeza kwa namna ambavyo amekuwa akitumia hekima na busara katika
kusikiliza na kushughulikia kero hizo. Baadhi ya malalamiko yanahitaji
uchunguzi wa kina, ili kubaini ukweli kabla ya kuchukua hatua, badala ya kutoa
maamuzi ya haraka yanayoweza kusababisha uonevu au kudhalilishwa kwa watumishi
wa umma.
Ni muhimu
kutambua kuwa, baadhi ya changamoto zinazowasilishwa na wananchi zinahitaji
ufafanuzi wa kiutendaji, nyingine zinahusu masuala ya kisheria, hivyo zinapaswa
kushughulikiwa kwa kuzingatia mazingira na taratibu husika. Hili ni jambo
ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa akilizingatia, tofauti na baadhi ya
viongozi wanaoweza kutumia malalamiko ya wananchi kama mtaji wa kisiasa na
kutoa maagizo bila kupima kwa kina mazingira na uhalisia wa jambo
linalowasilishwa.
Katika ziara
zake, Waziri Mkuu amekuwa akiambatana na baadhi ya Mawaziri, hususan wale
wanaosimamia sekta zinazogusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi.
Mara kadhaa amekuwa akitoa maelekezo ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza
papo hapo au kuchukua hatua stahiki kulingana na uzito au aina ya tatizo.
Akiwa mkoani
Shinyanga, Waziri Mkuu ametembelea halmashauri zote sita za mkoa huo, ambazo ni
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Manispaa
ya Shinyanga, Manispaa ya Kahama, Halmashauri ya Ushetu na Halmashauri ya
Msalala.
Katika
maeneo yote aliyotembelea, ametoa maagizo mbalimbali kwa watendaji wa Serikali.
Baadhi yanahusu changamoto mahususi za maeneo husika, huku mengine yakigusa
masuala ya kitaifa.
Katika
maoni haya, ninajikita zaidi katika baadhi ya maagizo yanayogusa masuala ya kitaifa na nitaanza
na yanayohusu sekta nyeti ya afya.
Miongoni mwa
maagizo aliyoyatoa katika Sekta ya Afya ni kupiga
marufuku hospitali za umma na vituo vyote vya kutolea huduma za afya
kuwachangisha fedha ya kununua mafuta ya gari la wagonjwa ndugu za wagonjwa
wanaopewa rufaa kwenda Hospitali nyingine hasa katika mazingira ya dharura.
Waziri Mkuu
alieleza kuwa, Serikali hutenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa magari hayo na
kuajiri madereva wanaolipwa mishahara.
Hivyo,
hakuna sababu ya ndugu wa wagonjwa kubebeshwa gharama za mafuta pale
wanapohitaji huduma ya usafiri wa dharura baada ya kupewa rufaa.
Alibainisha
kuwa, utaratibu huo umekuwa ukisababisha ucheleweshaji wa huduma na kuhatarisha
maisha ya wagonjwa hasa wanaohitaji matibabu ya haraka. Aliwataka viongozi wa
hospitali, vituo vya afya na zahanati kuhakikisha magari ya wagonjwa yanakuwa
na mafuta wakati wote, ili yaweze kutoa huduma mara moja pindi dharura
inapojitokeza.
Agizo jingine muhimu linahusu utoaji
wa huduma kwa wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka. Waziri Mkuu amewaelekeza watoa
huduma katika sekta ya afya kuhakikisha makundi hayo yanapatiwa huduma mara
moja pindi tu wanapofika kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali, bila
kucheleweshwa kwa sababu ya kufuata taratibu za kiutawala.
Alisisitiza
kuwa, utaratibu wa kuwasubirisha wajawazito na wagonjwa wa dharura mapokezi
haupaswi kuendelea na badala yake, wahudumiwe kwanza ili kuokoa maisha, huku
taratibu nyingine zinazotakiwa zikikamilishwa baadaye.
Alieleza
kuwa, kuendeleza utaratibu huo ni mazoea na uzembe unaoweza kusababisha vifo
vinavyoweza kuzuilika. Alitolea mfano mama mjamzito anayefikishwa hospitalini
akiwa na uchungu wa kujifungua, lakini anacheleweshwa kupata huduma kwa
kuulizwa mahitaji mbalimbali, yakiwemo vifaa vidogo kama beseni badala ya
kuhudumiwa kwanza.
Aliitaja
hali hiyo kuwa inaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto kwa sababu tu ya
mazoea ya watoa huduma.
Aidha,
alitoa agizo kwa viongozi na watendaji wa sekta ya afya, hospitali za umma na
vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha dawa wanazozihitaji wananchi zinapatikana,
badala ya kuambiwa wakanunue nje ya Hospitali.
Waziri Mkuu
alieleza kushangazwa na hali hiyo ambayo wamekuwa wakiilalamikia wananchi na
kubainisha kuwa, taarifa za utoshelevu wa dawa katika Hospitali na vituo vya
kutolea huduma za afya mara zote zinaonyesha kuwa ni zaidi ya asilimia 90,
lakini wananchi wanapofika kupata huduma, wanaelekezwa kununua dawa katika
maduka binafsi.
Alielekeza mamlaka
zinazohusika kudhibiti tabia hiyo, kwa vile haiendani na uwekezaji mkubwa ambao
Serikali imefanya katika kuboresha utoaji wa huduma kwenye Sekta ya afya.
Aliwataka
wale wanaohusika kuagiza dawa kwa ajili ya Hospitali na vituo vya kutolea
huduma za afya, wahakikishe wanaagiza dawa zote kulingana na mahitaji ya
wananchi wa eneo lao.
Waziri Mkuu pia alimuagiza Waziri wa
Mambo ya Ndani ya nchi Paschal Patrobas Katambi, kuhakikisha Jeshi la Polisi
kitengo cha usalama barabarani haliendelei na utaratibu wa kushikilia vyombo
vya moto vya wananchi waliofanya makosa ambayo adhabu yake ni faini, na kuvilundika
katika vituo vya Polisi.
Alisema utaratibu
huo unawasababishia wananchi hasara kubwa ikiwemo vyombo vyao kuharibikia
kwenye vituo vya Polisi, pamoja na kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo, kwa kuwa wanavitegemea vyombo hivyo katika kujiingizia kipato.
Waziri mkuu alielekeza kwamba, Polisi hawapaswi kushikilia vyombo vya wale wanafanya makosa yenye faini na badala yake wawaelekeze utaratibu unatakiwa kufuatwa kulipa faini hizo, huku wakiendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Katika kuyawekea uzito maagizo
yake, aliwaonya
watendaji wanaoweza kuyapuuza kwa madai kuwa ni kauli za kisiasa, akibainisha
kuwa, watakaobainika kwenda kinyume na maelekezo hayo watachukuliwa hatua.
Kwa mtazamo wangu, maagizo hayo ni muhimu na yanaonesha
namna Serikali inavyoguswa na changamoto zinazowakabili wananchi.
Hata hivyo, kutoa maagizo pekee hakutoshi kuleta
mabadiliko yanayotarajiwa, ikiwa hakutakuwa na mfumo madhubuti wa kuhakikisha
yanatekelezwa.
Bila
ufuatiliaji wa kina, maagizo hayo yanaweza kubaki bila kuleta matokeo yanayotarajiwa katika maisha ya
wananchi. Hali hiyo inaweza hata kuimarisha mtazamo wa baadhi ya watu kwamba,
maagizo hayo ni ya kisiasa na hayana dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko.
Ili kuzuia
hali hiyo, nashauri Ofisi ya Waziri Mkuu kuweka utaratibu maalumu wa kufuatilia
utekelezaji wa maagizo anayoyatoa kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na wilaya
pamoja na viongozi wengine.
Watendaji
wanaobainika kuyakiuka wachukuliwe hatua kali za kinidhamu. Wakuu au wasimamizi wa Idara husika ambao watashindwa
kusimamia ipasavyo maagizo hayo wachukuliwe hatua ili kuongeza uwajibikaji
kwenye taasisi za umma.
Kwa upande wa Sekta ya afya, nashauri kila hospitali na kituo cha kutolea huduma za afya kuwekwa mabango yanayoonekana kwa urahisi, yakiwa na namba maalumu za mawasiliano ya viongozi wa mkoa na wilaya ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na viongozi wengine wa maeneo husika.
Namba hizo zitawawezesha wananchi kutoa
taarifa wanapofanyiwa jambo kinyume na maelekezo ya Serikali, kuombwa fedha au
kucheleweshewa huduma bila sababu za msingi.
Utaratibu
huo utasaidia kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ushiriki wa wananchi katika
kufuatilia ubora wa huduma na kutoa nafasi kwa viongozi kupata taarifa za moja
kwa moja kuhusu ukiukwaji unaofanyika katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ni muhimu kukumbuka kuwa, imani kubwa ambayo wananchi
waliijenga kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli,
ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na namna alivyokuwa akifuatilia utekelezaji wa
maagizo aliyokuwa akiyatoa, ambapo wale waliokwenda kinyume chake walikiona cha
mtemakuni.
Mtindo huo
uliimarisha uwajibikaji kwa watendaji wa umma na kuwafanya wengi kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.
Kwa mantiki
hiyo, ninasisitiza kuwa, thamani ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Nchemba itapimwa
kwa mabadiliko yatakayopatikana katika utoaji wa huduma kwa wananchi.


0 Comments