Kwanza kabisa, niwapongeze wabunge wa viti maalumu ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao vizuri kwa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Wapo ambao wameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi na uwajibikaji, kiasi cha kufanya vizuri kuwazidi hata ya baadhi ya wabunge waliochaguliwa kupitia majimbo ya uchaguzi.
Mchango huo unathibitisha umuhimu wa nafasi ya ubunge wa viti maalumu, hususan katika kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi na vyombo vya maamuzi.
Kwa muda
mrefu, wanawake wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo mbalimbali vya kijamii
vilivyopunguza nafasi zao za kushiriki kikamilifu katika uongozi, licha ya kuwa
na mchango mkubwa katika malezi ya familia na ustawi wa jamii na taifa.
Kwa hakika, nafasi ya ubunge wa viti maalumu imekuwa jukwaa muhimu kwa wanawake kuonyesha uwezo wao katika uongozi na utumishi wa umma.
Baadhi yao wameitumia vizuri
nafasi hiyo na kujenga ushawishi mkubwa katika jamii, huku wengine wakitumia
uzoefu walioupata kugombea majimbo ya uchaguzi na kushinda dhidi ya wagombea
wanaume.
Hata hivyo,
pamoja na mafanikio hayo, bado wapo baadhi ya wabunge wa viti maalumu ambao
hawajaitumia nafasi hiyo ipasavyo, hasa katika kushughulikia changamoto
zinazowakabili wananchi katika maeneo wanayopaswa kuyawakilisha.
Kabla ya
kuangazia changamoto hiyo, ni muhimu kuelewa kwa ufupi historia na madhumuni ya
kuanzishwa kwa mfumo wa ubunge wa viti maalumu nchini Tanzania.
Mfumo wa
viti maalumu vya wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ulianzishwa mwaka 1992 kwa lengo la kuongeza uwakilishi wa wanawake katika
chombo hicho cha kutunga sheria, kutokana na idadi ndogo ya wanawake waliokuwa
wakifanikiwa kupata nafasi kupitia uchaguzi wa majimbo.
Hatua hiyo
ililenga kupanua ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi ya kitaifa,
kuhakikisha mahitaji na mitazamo yao yanazingatiwa katika mijadala na utungaji
wa sheria, pamoja na kukuza usawa wa kijinsia katika uwakilishi wa kisiasa.
Wabunge wa
viti maalumu hawachaguliwi moja kwa moja na wananchi kupitia majimbo ya
uchaguzi kama ilivyo kwa wabunge wa majimbo. Badala yake, hupatikana kupitia
utaratibu maalumu unaozingatia uwakilishi wa vyama vya siasa bungeni na
masharti ya Katiba na sheria za uchaguzi.
Kwa
utaratibu huo, vyama vya siasa vinavyostahili hupata nafasi za viti maalumu
kulingana na uwiano wa uwakilishi wao, kisha kuwasilisha majina ya wanawake
wanaopendekezwa kupitia utaratibu wa ndani ya vyama kujaza nafasi hizo, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Jambo muhimu
la kuelewa ni kwamba, Mbunge wa viti maalumu ana hadhi na mamlaka ya kibunge
kama alivyo mbunge wa jimbo. Tofauti yao kubwa ipo katika namna
wanavyopatikana, siyo katika umuhimu wa nafasi zao wala wajibu wao wa kibunge.
Majukumu yao
yanajumuisha kutunga sheria, kuishauri na kuisimamia Serikali, kushiriki katika
mijadala na kupitisha bajeti, kuwasilisha changamoto na maoni ya wananchi
bungeni, kutetea haki na usawa wa kijinsia, pamoja na kufuatilia masuala
mbalimbali ya kijamii na kiuchumi yanayohitaji ufumbuzi.
Hivyo,
pamoja na kutekeleza majukumu yao ndani ya Bunge, wanapaswa pia kuwa karibu na
wananchi, kuwasikiliza, kutambua changamoto zao na kuzifikisha katika vyombo
husika vya maamuzi ili zipatiwe ufumbuzi.
Hapa ndipo
ninapoona kuna changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi. Baadhi ya wabunge wa viti
maalumu hawaonekani kuwa karibu na wananchi wala kushiriki kwa ukamilifu katika
kushughulikia kero zinazowakabili, licha ya nafasi na wigo mpana wa uwakilishi
walionao.
Cha
kusikitisha zaidi, wapo ambao wananchi katika maeneo wanayotoka hawawafahamu
vizuri, wala hawajui wanakopatikana. Mara nyingi huwaona kwenye matukio maalumu, shughuli za vyama na majukwaa ya
mikutano ya viongozi wa kitaifa wanapotembelea maeneo yao, ambapo nao hupewa
nafasi ya kuzungumza na kutumia fursa hiyo kujitambulisha kama wageni na baadaye kuanza kueleza changamoto za wananchi ambao wakati mwingine
hawajapata hata fursa ya kukutana nao.
Kupitia
maoni haya, ninawashauri wabunge wa viti maalumu wajenge utaratibu wa
kutembelea maeneo wanayoyawakilisha, kukutana na wananchi, makundi wanayoyawakilisha na hasa wanawake,
kusikiliza changamoto zao na kushirikiana na wabunge wa majimbo kutafuta
ufumbuzi. Hawapaswi kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa ili wapate nafasi ya
kuzungumza na wananchi au kuonyesha uwepo wao.
Wananchi
wanahitaji kuwaona na kuwasikia wawakilishi wao mara kwa mara, siyo kuwafahamu
kupitia matangazo ya Bunge pekee. Mbunge anayewajibika anapaswa kutambulika kwa
kazi anazozifanya na matokeo anayoyaleta katika jamii, siyo kwa nafasi
aliyonayo au hotuba anazotoa kwenye mikutano ya hadhara.
Ukweli ni
kwamba, wapo wabunge wa viti maalumu ambao wamejenga uhusiano wa karibu na
jamii kiasi kwamba majina yao yanatambulika vizuri katika maeneo
wanayoyawakilisha. Hata ukiwauliza watoto wanawafahamu vizuri kutokana na shughuli na mchango
wao. Hii inaonyesha kuwa nafasi hiyo inaweza kutumika kuleta mabadiliko makubwa
endapo mhusika atakuwa na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
Kwa mfano, Dkt. Dorothy Gwajima ambaye kwa sasa ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya jamii, wanawake na makundi maalum, licha ya kuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais, amekuwa akifanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla, jambo lililomfanya kufahamika na kutambulika kutokana na kazi zake.
Mbali na Dkt. Doroth Gwajima, wapo wabunge wengine wa Chama tawala na vyama vya upinzani ambao
waliingia bungeni kupitia viti maalum vya wanawake ambao wanafahamika kwa
mchango mkubwa kwenye taifa na jamii na wameacha alama isiyofutika.
Hata hivyo,
bado wapo baadhi ya wabunge ambao mchango wao katika jamii hauonekani wazi, na
hata ndani ya Bunge wamekuwa wakijikita zaidi katika kuunga mkono hoja za
wengine badala ya kuibua hoja, kupendekeza suluhisho na kusimamia masuala
yanayogusa maisha ya wananchi ikiwemo kundi wanaloliwakilisha. Wamekuwa kama wamepewa Ubunge wa peke yao au sehemu tu ya ajira na siyo uwakilishi.
Ninatoa wito kwa wabunge wote wa viti maalumu kubadili mtazamo huo na kutambua kwamba, nafasi walizonazo ni dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Wanapaswa kuwa sehemu ya
suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi na siyo kutegemea wabunge wa
majimbo pekee kubeba jukumu hilo.
Aidha,
ninawashauri viongozi wa kitaifa wanapotembelea maeneo mbalimbali nchini, kabla
ya kuwapa vipaza sauti wawapime kwanza kwa kuwauliza wananchi wa maeneo wanayotoka kama wanawafahamu.
Hatua hiyo inaweza kusaidia kuongeza uwajibikaji na kuwafanya wabunge hao
wajitathmini kuhusu namna wanavyotekeleza majukumu yao.
Ni muhimu
kuelewa kuwa, nafasi ya ubunge wa viti maalumu haikuanzishwa kwa ajili ya
kuongeza idadi ya wanawake bungeni pekee, bali pia kuhakikisha wanashiriki
kikamilifu katika maamuzi na kuleta mabadiliko katika jamii.
Wanawake hawawezi kunufaika kikamilifu na nafasi walizopigania ikiwa baadhi ya wanaopewa dhamana ya kuwawakilisha hawataitumia ipasavyo.
Wabunge wa viti maalumu wanapaswa kuwa karibu na wananchi na washirika wa wabunge wa majimbo katika kutatua kero za wananchi, na kutumia fursa hiyo kuonyesha uwezo wao ili jamii iendelee kuwaamini kwenye uongozi na kuondoa mitazamo inayowatweza wanawake.

0 Comments