Makamu wa Rais Mteule, Deogratius Ndejembi
Makamu wa Rais Mteule, Deogratius Ndejembi, amethibitishwa
na Bunge leo Agosti 28, 2026 katika Kikao cha Tatu cha Mkutano wa Nne wa Bunge
la 13, akiahidi kuwa mtii kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akiwashukuru wabunge baada ya kumthibitisha, Ndejembi mesema anatambua kuwa, jukumu alilopewa sio la kwake peke yake bali ni kwa ajili ya Watanzania wote.
Aidha, amesema atakuwa Makamu wa Rais wa Watanzania wote, bila ubaguzi wa itikadi za vyama na amekishukuru chama chake cha CCM, akisema kimeonesha imani kubwa kwa vijana na kwamba uteuzi wake, umedhihirisha namna chama hicho kinavyowalea vijana na kuwapika kuwaandaa kushika nyadhifa kubwa.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamemthibitisha Ndejembi kuwa Makamu wa Rais kwa kura zote 324 zilizopigwa, huku hakuna kura ya hapana wala iliyoharibika.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Ndejembi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpa nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo kuwa Naibu Waziri na Waziri katika Wizara tofauti.
Ndejembi amethibitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais, baada ya aliyekuwa kwenye nafasi hiyo, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kujiuzulu kwa kuandika barua Agosti 25, 2026.
Kabla ya kupendekezwa kuwa Makamu wa rais, Ndejembi alikuwa Waziri wa Nishati.

0 Comments