Ajali za barabarani nchini Tanzania zimekuwa zikigharimu
maisha ya watu, kusababisha majeruhi na kuwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.
Nyuma ya kila kifo au ulemavu kuna familia inayobeba maumivu makubwa ya madhara
au kumpoteza mtu waliyemtegemea, mlezi au waliyempenda.
Ingawa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupitia
Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, bado ajali zinaendelea kutokea.
Hii inaonyesha kuwa, juhudi zaidi zinahitajika na hasa katika usimamizi wa
sheria.
Tatizo kubwa ni baadhi ya watumiaji wa barabara, hasa
madereva, kupuuza sheria kwa kuendesha kwa mwendo kasi, kuvuka magari yaliyoko
mbele yao bila kuchukua tahadhari (overtaking) katika maeneo hatarishi na
kuendesha bila kuzingatia usalama wa wengine.
Mtu anayesafiri mara kwa mara anaweza kushuhudia baadhi ya madereva wakifanya vitendo vya hatari, ikiwemo kupita magari katika kona au maeneo ambayo hawawezi kuona mbele kwa usalama. Kinachotia hofu zaidi ni pale dereva anapokaribia kusababisha ajali badala ya kutafakari uzembe alioufanya, anaona ni jambo la kawaida na kurudia kosa lile au wakati mwingine kucheka.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga
Agosti 27, 2026, inaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makosa 5,291 ya ukiukaji wa
sheria za usalama barabarani yalibainika mkoani Shinyanga katika kipindi cha
Juni hadi Agosti 27, 2026. Kati yake, makosa 4,079 yalihusu magari, huku 1,212
yakihusu bajaji na pikipiki.
Ingawa taarifa hiyo haikubainisha ni makosa mangapi
yalisababisha madhara, idadi hiyo inaonyesha wazi kuwa bado kuna changamoto
kubwa katika uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani.
Idadi hii, katika mkoa mmoja na ndani ya kipindi kifupi,
inapaswa kuwa kengele ya tahadhari. Haiwezi kuchukuliwa kama takwimu za kawaida.
Kutokana na hali hiyo, nashauri Serikali
kupitia Wizara ya mambo ya ndani kuongeza nguvu kwenye rasilimali
na bajeti kwa Kikosi cha Usalama Barabarani, ili kiwe na uwezo wa kufanya
doria, ukaguzi na utekelezaji wa sheria kwa ufanisi zaidi.
Pia, mpango wa kutumia kamera za ufuatiliaji katika
barabara kuu na za masafa marefu unapaswa kupewa kipaumbele. Teknolojia inaweza
kusaidia kubaini mwendo kasi na ukiukaji mwingine wa sheria, huku ikipunguza
utegemezi wa askari kulazimika kudhibiti kila tukio kwa njia ya kawaida ya
kusimama barabarani. Ushahidi wa kamera unaweza kusaidia kuongeza uwajibikaji
na kupunguza mianya ya rushwa.
Kwa madereva wanaokiuka sheria mara kwa mara, ni wakati sasa
wa kuweka mfumo madhubuti wa kurekodi makosa yao na kuchukua hatua kulingana na
uzito na marudio ya makosa.
Hatua hizo zinaweza kujumuisha kusimamishwa kuendesha
kwa muda, faini kubwa na pale inapobidi kufungiwa leseni kwa mujibu wa sheria,
ingawa suala la kumfungia leseni linapaswa kuwa chaguo la mwisho kwa kuzingatia
pia madhara kwa watu wengine wanaomtegemea.
Abiria nao wanapaswa kutambua kuwa, wana wajibu wa kukataa
kuwa watazamaji. Dereva anapoendesha kwa namna inayohatarisha maisha, abiria
wanapaswa kuwa na ujasiri wa kumtaka apunguze mwendo au kutoa taarifa kwa
mamlaka husika. Usalama wa abiria haupaswi kuishia kwenye kulipa nauli.
Waendesha pikipiki na bajaji pia wanapaswa kuzingatia
sheria. Kasi isiyodhibitiwa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu si uhodari,
bali ni hatari inayoweza kugharimu maisha yao na ya watu wengine.
Sote tunapaswa kutambua kuwa, barabara
si uwanja wa mashindano. Kila dereva anayekanyaga mafuta kupita
kiasi, anayefanya overtaking kwa uzembe au anayepuuza sheria anaweka maisha
yake na ya wengine rehani, “Tukifa haturudi”
Serikali, madereva, waendesha pikipiki na bajaji, abiria na
watumiaji wengine wa barabara wanapaswa kuchukua jukumu lao.
Hatupaswi kusubiri
msiba utupate ndipo tukumbuke thamani ya maisha. Kuzuia ajali ni bora kuliko kuomboleza baada ya ajali.
0 Comments