SERIKALI YAZITAKA TAASISI ZOTE KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI YA KUNYONYESHEA

 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara ya Kinga na Lishe, imezitaka taasisi za umma na binafsi kuweka na kuimarisha mazingira rafiki yatakayowawezesha akina mama kuendelea kunyonyesha watoto wao hata wanapokuwa kazini.

Wito huo umetolewa Agosti 7, 2026, na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya, Bi. Amisa Mwakawago, wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani 2026 na kuzindua chumba maalum cha unyonyeshaji katika Ofisi za Wizara ya Afya, Mtumba, jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu “Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto Huanza na Maziwa ya Mama.”

Bi. Mwakawago amesema uzinduzi wa chumba hicho unaonesha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwawezesha wanawake kuendelea kunyonyesha watoto wao baada ya kurejea kazini.

Amesema unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ni miongoni mwa afua zenye matokeo makubwa katika kuokoa maisha ya watoto, kuimarisha kinga ya mwili, kuboresha lishe na kuchangia ukuaji na maendeleo ya ubongo.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliud Eliakimu, amesema mafanikio katika unyonyeshaji yanahitaji ushirikiano wa familia, jamii, watoa huduma za afya, waajiri na wadau wa maendeleo.

Amesisitiza umuhimu wa kumwezesha mama kuanza kunyonyesha mapema, kumpa mtoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza na kuendelea kunyonyesha hadi mtoto atimize miaka miwili au zaidi, sambamba na kumpatia lishe bora ya nyongeza.

Dkt. Eliakimu pia amehimiza kuunganishwa kwa huduma za unyonyeshaji na huduma za malezi na makuzi ya awali ya mtoto, ikiwemo kuwapatia wazazi na walezi elimu kuhusu malezi yenye upendo, mawasiliano chanya na matumizi ya michezo katika kujifunza.

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kujenga msingi imara wa ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Kinga, Sehemu ya Epidemiolojia, Dkt. Vida Mmbaga, amezitaka taasisi za umma na binafsi kuanzisha na kuimarisha vyumba vya unyonyeshaji pamoja na kuweka sera rafiki kwa wazazi mahali pa kazi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda haki ya mtoto kupata maziwa ya mama, huku ikimuwezesha mama kutekeleza majukumu yake ya kikazi kwa ufanisi.

Dkt. Mmbaga amesisitiza kuwa uwekezaji katika unyonyeshaji ni sehemu muhimu ya uwekezaji katika afya ya jamii na maendeleo ya Taifa.

Imeandikwa na Andrea Kadege, Wizara Afya – Dodoma

 

 


Post a Comment

0 Comments