WHO YATOA WITO KUONGEZA KASI YA KUKABILIANA NA EBOLA DRC

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, idadi ya visa vya Ebola imevuka 4,000, huku mlipuko huo ukitajwa kuwa wa pili kwa ukubwa zaidi kuwahi kurekodiwa duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa wito wa kuongeza kasi ya kukabiliana na mlipuko huo na kusema kwamba Ebola inaweza kudhibitiwa.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na hatua nyingine ya kutisha katika mlipuko wake wa Ebola, baada ya idadi ya visa vilivyothibitishwa kuvuka 4,000 kwa mara ya kwanza, huku kukiwa na hofu mpya kwamba virusi hivyo vinaweza kusogea karibu na mji mkuu Kinshasa.

Takwimu za hivi karibuni za taasisi ya afya ya umma ya DRC zinaonyesha visa 4,053 vimethibitishwa, na watu 1,850 wamefariki dunia.

Huu ni mlipuko wa pili kwa ukubwa zaidi kuwahi kurekodiwa duniani, baada ya ule wa Afrika Magharibi wa mwaka 2014 hadi 2016 uliokuwa na zaidi ya visa 28,000.

Mlipuko wa sasa umeenea katika majimbo matano ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Haut-Uele na Tshopo, huku Ituri ndiyo kitovu kikuu.

Lakini wasiwasi umeongezeka zaidi baada ya mtu anayeshukiwa kuwa na  Ebola kufariki ndani ya boti iliyokuwa ikielekea Kinshasa kutoka Tshopo.

Mamlaka ziliifuatilia boti hiyo na kuizuia umbali wa kilomita 65 kutoka Kinshasa, mji wenye wakazi karibu milioni 17.

Maabara inayohamishika imepelekwa eneo hilo kuwapima abiria wote, huku boti ikiendelea kutengwa.

Post a Comment

0 Comments