Wakazi wa maeneo ya Mageuzi, Dodoma, Butengwa na Ndembezi (Mwanoni) katika Manispaa ya Shinyanga wamepongeza hatua ya Serikali ya
kukamilisha ujenzi wa Daraja la Dodoma, linalounganisha Mtaa wa Mageuzi, Kata
ya Ngokolo na Mtaa wa Butengwa, Kata ya Ndembezi.
Wananchi hao wamesema kukamilika kwa daraja hilo kumeondoa
adha waliyokuwa wakiipata kwa muda mrefu, hususan wakati wa masika, ambapo
eneo hilo lilikuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi waliokuwa wakivuka kutoka
upande mmoja kwenda mwingine.
Wameeleza kuwa daraja hilo litachangia kuharakisha shughuli
za maendeleo katika maeneo hayo, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo
walilazimika kuvuka kwa shida walipokuwa wakielekea kwenye shughuli zao za kila
siku, na wakati mwingine kuzunguka umbali mrefu ili kuepuka hatari ya kusombwa
na maji.
Katika hatua nyingine, wananchi hao wameiomba Serikali
kupitia Wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) kutumia kipindi hiki
cha kiangazi kuweka changarawe kwenye barabara zilizochongwa hivi karibuni
katika maeneo hayo, pamoja na kujenga makalavati kwenye maeneo korofi ili
kuwaondolea usumbufu wakati wa mvua.
Aidha, wameomba Serikali kuendelea kufungua barabara katika
maeneo ambayo bado hayajafikiwa, ili kuhakikisha maeneo yote yenye makazi ya
watu yanapitika kwa urahisi.
Mradi wa ujenzi wa Daraja la Dodoma ulianza kutekelezwa
tarehe 15 Desemba 2025 na Kampuni ya Sabu Enterprises Co. Limited ya
mkoani Shinyanga, chini ya usimamizi wa Kampuni ya Norplan Tanzania Limited
ya Dar es Salaam.
Mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 105 hadi
kukamilika kwake.
Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Samson Pamphili, daraja hilo limekamilika kwa asilimia 100 na linatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 19 Agosti 2026, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Shinyanga.
Daraja la Dodoma limewahi kutajwa na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Patrobas Katambi, kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyowagusa moja kwa moja wananchi wa Shinyanga kupitia utekelezaji wa miradi iliyopewa kipaumbele katika siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
0 Comments