ALLY’S STAR YAJA NA SULUHISHO CHANGAMOTO YA MABASI KUKOMEA STENDI YA MAGUFULI

Kampuni ya mabasi ya Ally’s Star yenye makao makuu mjini Shinyanga, imewahakikishia wananchi kuwa, mabadiliko ya utaratibu wa mabasi ya abiria kuishia katika Stendi Kuu ya Magufuli, Mbezi Luis, hayatasababisha usumbufu kwa wateja wake.

Meneja wa Kampuni hiyo, Bw. Abita Iman, ameiambia SHINYANGA ONE kuwa, kampuni imejipanga kwa kuandaa magari maalum ya kuwachukua abiria kutoka Stendi Kuu ya Magufuli na kuwapeleka hadi katika ofisi zake zilizopo Manzese Argentina.

Amesema utaratibu huo umelenga kurahisisha usafiri kwa abiria wanaohitaji kwenda maeneo mbalimbali, ikiwemo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Meneja wa Kampuni ya Ally's Star, Bw. Abita Iman

Aidha, amesema kampuni imeweka utaratibu wa kuwachukua na kuwapeleka hadi Stendi Kuu ya Magufuli abiria wanaokata tiketi kupitia ofisi za Ally’s Star zilizopo Manzese Argentina, ili kuwaondolea usumbufu wa kutafuta usafiri mwingine.

Ofisi za kampuni ya Ally's Star zilizopo Manzese Argentina Jijini Dar es salaam

Kwa upande wa abiria wanaosafiri kwenda Mwanza na kushukia Stendi ya Nyegezi, Iman amesema kampuni imeandaa usafiri maalum wa kuwafikisha katikati ya Jiji la Mwanza, kupitia ofisi zake zilizopo eneo la Nata.

Iman amewaomba wananchi, wakiwemo wakazi wa Shinyanga, kuendelea kuiamini kampuni hiyo, akisema inatoa huduma kwa kuzingatia mahitaji ya wateja pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha hawapati usumbufu kutokana na mabadiliko ya utaratibu wa usafiri.

Ally’s Star, inayomilikiwa na wawekezaji wazawa kutoka mkoani Shinyanga, hutoa huduma za usafirishaji wa abiria kwa safari za masafa marefu na mafupi katika maeneo mbalimbali nchini.

Safari za kampuni hiyo zinahusisha mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Mwanza, Mara, Simiyu, Usinge Tabora, Iringa, Mbeya, Katavi na Rukwa.

Bw. Abita Iman akiwa Ofisini kwake

Ofisi za makao makuu ya Kampuni ya Ally's Star mjini Shinyanga


Post a Comment

1 Comments