Kwanza
kabisa, ninaipongeza Serikali kwa maono na jitihada zake za kuhakikisha
Watanzania wote, bila kujali hali zao za kiuchumi au matabaka yao, wanapata
fursa ya kupata huduma bora za afya kupitia mpango iliouanzisha wa Bima ya Afya
kwa Wote.
Hatua hii ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na inaweza kusaidia kuokoa maisha ya wananchi ambao wakati mwingine hushindwa kupata matibabu kwa sababu ya kukosa fedha, hususan wanapokabiliwa na magonjwa yanayohitaji gharama kubwa za matibabu.
Pia, ninaipongeza Serikali kwa hatua iliyofikia katika utekelezaji wa mpango huo kwa awamu ya kwanza, kwa kuanza kuwahudumia wananchi kutoka katika kaya zisizo na uwezo ambao pia ni wanufaika wa TASAF.
Hatua hiyo ambayo inakwenda pamoja na serikali kugharamia bima za afya kwa kundi hilo la watu wasiokuwa na uwezo, inaonyesha dhamira ya Serikali ya kulinda afya na ustawi wa wananchi wote na kuwapa kipaumbele wale ambao wana uhitaji zaidi.
Hata hivyo, Serikali inapaswa kutambua kwamba, si kila mwananchi ambaye si mnufaika wa TASAF ana uwezo wa kumudu gharama za matibabu nje ya bima ya afya kwa wote, hivyo, mchakato wa kuhakikisha watanzania wote wanakuwa na bima ya afya unapaswa kuharakishwa ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za matibabu.
Itambulike kwamba, bado kuna idadi kubwa ya wananchi ambao huchelewa kwenda hospitalini au kuamua kubaki nyumbani, huku wakikabiliwa na changamoto za kiafya kwa sababu tu ya kutokuwa na uwezo wa kugharamia huduma za matibabu na hasa kwa magonjwa ambayo matibabu yake yanahitaji gharama kubwa.
Hali hii ni hatari kwa wagonjwa hasa wanaohitaji matibabu ya haraka na imekuwa ikisababisha madhara makubwa kwa afya na kuhatarisha maisha yao.
Hatua ya watanzania wote kuwa na Bima ya Afya itasaidia kuharakisha utolewaji wa huduma kwa wagonjwa, tofauti na ilivyo sasa ambapo wakati mwingine mgonjwa hulazimika kusubiri kwa muda mrefu mapokezi hadi taratibu za malipo zikamilike, au baadhi ya huduma kutotolewa mpaka pale malipo yatakapofanyika, hali ambayo ni hatari hasa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.
Bima ya Afya kwa wote pia inaweza kusaidia kupunguza changamoto ambazo baadhi ya familia hukutana nazo baada ya kumpoteza ndugu yao huku kukiwa na madai ya gharama za matibabu ambazo hazijalipwa, hali ambayo wakati mwingine husababisha mwili wa marehemu kushikiliwa hospitali mpaka madeni hayo yalipwe.
Hali hiyo inaongeza mzigo na maumivu kwa familia ambayo tayari iko kwenye kipindi kigumu cha majonzi ya kumpoteza mpendwa wao, huku tena ikikabiliana na gharama nyingine za kusafirisha mwili, gharama za mazishi na deni la matibabu ya marehemu wanalotakiwa kulilipa.
Vilevile, mfumo wa bima ya afya kwa wote unaweza kusaidia kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za afya, kwa sababu utaleta ushindani hasa kwa watoa huduma binafsi ili kuvutia watu wengi kwenda kwenye vituo vyao vya kutolea huduma.
Takwimu zitakazopatikana kupitia matumizi ya mfumo wa bima ya afya kwa
wote zinaweza kusaidia Serikali, kufanya ufuatiliaji, kufahamu namna huduma
zinavyotolewa na mapungufu hasa kwa Hospitali za umma, kujua huduma
zinazohitajika zaidi, kubaini maeneo yanayohitaji uwekezaji zaidi na kupanga
raslimali.
Kuhusu gharama ya Bima ya Afya kwa Wote zilizowahi kutajwa kwa familia ya watu sita kwa mwaka, yaani mwanachama mchangiaji, mwenza wake na watoto wanne, ni nafuu sana ikilinganishwa na gharama ambazo familia inaweza kukutana nazo inapolazimika kugharamia matibabu moja kwa moja.
Na katika kuhakikisha wananchi wote wanajiunga na bima hiyo, Serikali inaweza kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu wa malipo kwa awamu, kwa mfano kama gharama ni shilingi 150,000/= kwa mwaka, mwanchi anatakiwa kuichangia mara mbili ndani ya mwaka husika, yaani mwanzoni mwa mwaka na kati kati ya mwaka, hatua ambayo itawawezesha hata wale wenye kipato cha chini kutoteteleka kulipa gharama hizo.
Hakuna mwananchi atakayeshindwa kujiunga na bima hiyo endapo ataelimishwa kwa kina kuhusu umuhimu wake, faida na unafuu wa gharama ambao ataupata ikilinganishwa na kulipa fedha moja kwa moja kila anapoungua.
Kwa msingi huo, naona umuhimu wa kuharakishwa kwa mchakato huo, hatua ambayo itawawezesha kulinda afya za wananchi kwa kupata huduma za kiafya kwa wakati na kwa gharama wanayoweza kiumudu.
Endapo kuna changamoto yoyote katika utekelezaji wake, ni vyema wananchi na wadau wengine wakashirikishwa ili kuona namna ya kupata suluhisho la pamoja.

0 Comments