HECHE AWAOMBA WANA SHINYANGA KUENDELEA KUIUNGA MKONO CHADEMA

 

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania bara, John Heche, amewaomba wananchi wa Shinyanga kuendelea kukiunga mkono chama hicho, katika juhudi zake za kupigania haki za watanzania

Akizungumza mjini Shinyanga leo Jumanne tarehe 22, Septemba, 2026, kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa JASCO, Heche amesema chama hicho bado kimesimama imara katika kutetea haki za wananchi, licha ya changamoto mbalimbali ambazo kinapitia  alizozitaja kuwa zina lengo la kutaka kuwanyamazisha.

Amesema chama hicho hakiwezi kurudi nyuma katika kuwapambania wanachi, licha ya kuandamwa na kupitia misukosuko mingi kutokana na kupigania haki za watanzania, hatua ambayo imelenga kukinyamazisha.

Amewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho  kutovunjika moyo wala kurudi nyuma na badala yake waendelee kukiunga mkono, ili kuhakikisha yale wanayoyapigania yanaleta manufaa kwa watanzania wote.

Kiongozi huyo wa upinzani amebainisha kuwa, CHADEMA kwa sasa imebeba Ajenda mbili muhimu, ikiwemo ya kupigania Katiba mpya ambayo itaondoa mifumo inayowaumiza wanachi, pamoja na Ajenda ya Free Tundulisu, ambayo imelenga kushinikiza kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Antipas Lisu, ambaye anashikiliwa na vyombo vya dola kwa kesi ya uhaini inayomkabili, kutokana na juhudi zake za kupigania haki za watanzania.

Heche amebainisha kuwa, endapo Katiba mpya itapatikana, itasaidia kuweka mifumo ambayo itawezesha kupata viongozi ambao watawajibika moja kwa moja kwa wananchi na kuwawezesha kunufaika na raslimali zilizopo.

Amesema viongozi wanaochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi wenyewe wanapaswa kuwa na uwezo wa kuibua na kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo ya wananchi, akitolea mfano Ziwa Victoria ambalo kwa mujibu wa maelezo yake, linaweza kutumika kuongeza fursa za kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yanayolizunguka ukiwemo mkoa wa Shinyanga.

Heche pia amezungumzia uwepo wa rasilimali za madini, hususan dhahabu na almasi, mkoani Shinyanga, akisema rasilimali hizo zinaweza kuwa chanzo cha maendeleo kwa wananchi iwapo zitatumika kwa mipango inayolenga kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa jamii.

Kuhusu zao la pamba, Heche amesema bei yake haitoshi kuwaondoa wananchi katika umaskini, akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya zao hilo kwa kuwekeza katika viwanda vitakavyosindika pamba na kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo.

Amesema hatua hiyo inaweza kuongeza thamani ya pamba na kutoa fursa za ajira kwa wananchi, wakiwemo wale wasio na kiwango kikubwa cha elimu.

Aidha, Heche amewaomba wananchi kuendelea kuchangia shughuli za chama kupitia kampeni ya “Tone Tone”, akisema michango hiyo itasaidia CHADEMA kuendesha shughuli zake na kwamba, kwa kufanya hivyo watakuwa wanashiriki shughuli za ukombozi.

SHINYANGA ONE MEDIA, imeshuhudia baadhi ya wanachama wa CHADEMA katika Manispaa ya Shinyanga wakitoa michango yao kupitia kampeni hiyo ya "Tone Tone"  kwa ajili ya kuwezesha shughuli za chama.

Post a Comment

0 Comments