WANAHABARI SHINYANGA WATAKIWA KUELIMISHA UMMA KUHUSU UMUHIMU MIRADI INAYOSIMAMIWA NA TPDC

 

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi


Waandishi wa habari mkoani Shinyanga,wametakiwa kutumia
nafasi waliyonayo kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu
wa miradi ya kimkakati ya mafuta na gesi, ikiwemo Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Akifungua mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Shinyanga, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, amesema waandishi wana wajibu wa kueleza kwa wananchi manufaa yanayotokana na miradi hiyo, pamoja na kuhamasisha jamii kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia miradi hiyo.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ili iwe sehemu muhimu ya kukuza uchumi wa Taifa na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa zinazotokana na miradi hiyo kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowanufaisha , huku wakishirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu ya miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa shirika kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia.

Amesema gesi asilia ni hitaji la muhimu kwa sasa , kwa sababu inatakiwa kwenye matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani, viwandani na kwenye vyombo vya usafiri, ambapoTPDC kwa kushirikiana na Serikali inaendelea na mikakati ya kuongeza wigo wa usambazaji wa nishati hiyo nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu

Akizungumzia Bomba la  EACOP, Kaimu Mratibu wa Mradi huo kutoka TPDC, Jumanne Mohamed, amesema utekelezaji wake unazingatia masuala ya mazingira na jamii, huku hatua mbalimbali zikichukuliwa kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza.

Amesema mafuta yatarajiwa kuanza kuingizwa kwenye bomba hilo ifikapo Januari 15, 2027 na kusafirishwa hadi kituo cha Chongoleani mkoani Tanga, ambapo wabia wote ikiwemo Uganda na Tanzania watanufaikana mradi huo.

Kwa mujibu wa Jumanne, mradi huo umepita katika mikoa minane ya Tanzania ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida,Dodoma, Manyara na Tanga.

Kaimu Mratibu wa Mradi wa EACOP kutoka TPDC, Jumanne Mohamed

Kwa upande wa mkoa wa Shinyanga, bomba hilo linalotokea nchini Uganda, limepita Wilayani Kahama kwenye vijiji na mitaa 16, ambapo kaya 10 zilizoathiriwa na utekelezaji wa mradi zimelipwa fidia, yenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 1.8.

Aidha, amebainisha kuwa, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, pia zinahusisha mkoa wa Shinyanga katika Bonde la Eyasi-Wembere kwenye eneo la Wilaya ya Kishapu.

Akizungumza kwa niaba ya wandishi wa Habari mara baada ya mufunzo  hayo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, ameishukuru TPDC kwa kuwapa mafunzo ambayo yamewaongezea uelewa na uwezo wa kuripoti kwa usahihi kuhusu sekta ya mafuta na gesi, miradi ya kimkakati pamoja na fursa zinazotokana na sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru

Shirika la maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni shirika la umma linalosimamia maendeleo ya raslimali za mafuta na Gesi asilia nchini,  ambapo pamoja na mambo mengine, linashiriki katika utafutaji wa mafuta na Gesi asilia, kuendeleza na kusimamia miradi ya mafuta na Gesi pamoja na kushiriki katika uzalishaji na biashara ya Gesi na mafuta.

Pia linasimamia miundombinu ya Gesi na mafuta, kuwakilisha maslahi ya Serikali katika uwekezaji kwenye Sekta ya mafuta na Gesi pamoja na kushirikiana na kampuni za ndani na kimataifa katika utafutaji na maendeleo ya raslimali hizo.

 

 

Post a Comment

0 Comments