POLISI ARUSHA YABAINI MBINU MPYA YA MTANDAO WA WEZI WA BODABODA

 

Uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha umebaini mbinu inayodaiwa kutumiwa na mtandao wa wahalifu, ambapo abiria walitumika kuwakodi madereva wa bodaboda na kuwaelekeza katika maeneo maalum yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili ya kutekeleza matukio ya uhalifu.

Katika hatua nyingine, polisi imemkamata mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitumiwa katika mpango huo, huku watu wengine sita wakikamatwa kwa nyakati tofauti kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao huo.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu, yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji na wizi wa pikipiki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jastine Masejo, uchunguzi umebaini kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali, yakiwemo baadhi yaliyotokea hivi karibuni.

Amesema watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani, huku mashauri yao yakiendelea katika hatua mbalimbali za kisheria.

“Miongoni mwa matukio hayo ni tukio la mauaji ya Anold Osward (28), mkazi wa Orolesho, Kata ya Olasiti, Jijini Arusha, lililotokea Juni 19, 2026 katika Mtaa wa Olteves, Kata ya Olmot, Jijini Arusha.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio la mauaji ya Hamis Masimba (22), dereva wa bodaboda na mkazi wa Olasiti, Jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Masimba alidaiwa kupotea Septemba 9, 2026 baada ya kumchukua abiria, kabla ya mwili wake kupatikana Septemba 12, 2026 ndani ya nyumba ambayo haijakamilika iliyopo katika eneo la Stendi Mpya, Mtaa wa Bondeni City, Jijini Arusha.

Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu na watu wanaodhaniwa kujihusisha na vitendo hivyo, ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Aidha, amewataka madereva wa bodaboda na wamiliki wa pikipiki kuwa makini wanapobeba abiria au kukodisha pikipiki zao, hususan nyakati za usiku, na kutoa taarifa mapema wanapobaini mwenendo wowote unaotia shaka.

SOURCE: IPP MEDIA
 

Post a Comment

0 Comments