TUJIFUNZE KUTOKA DODOMA NAMNA YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA ZA EL NIÑO

 

Ripoti ya Mwandishi wa Habari wa TARURA makao makuu Dodoma, Catherine Sungura, ambayo imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii imeeleza kuwa, viongozi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Dodoma, mkoani Dodoma, wamefanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara, ikiwemo madaraja, makalavati na mifereji, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Hatua hiyo imekuja kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, kuanzia mwishoni mwa mwezi Septemba, 2026.

TMA imeonya kuwa, mvua hizo zinaweza kusababisha athari mbalimbali, zikiwemo mafuriko na kukatika kwa mawasiliano, hivyo mamlaka na wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema.

Taarifa ya Catherine Sungura ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na mahusiano ya umma wa TARURA makao makuu, imeeleza kuwa, timu ya TARURA wilaya ya Dodoma imetembelea na kubaini mapema maeneo yenye viashiria vya hatari ili kuchukua hatua za kuyafanyia maboresho kabla mvua hazijaanza kwa nguvu, ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko, uharibifu wa barabara na miundombinu mingine.

Kwa mtazamo wangu, hatua iliyochukuliwa na TARURA Wilaya ya Dodoma inastahili kupongezwa, kwa sababu inaonyesha umuhimu wa kuchukua hatua za kinga kabla ya tatizo kutokea. Si busara kusubiri mvua kubwa zianze kunyesha, miundombinu iharibike na taharuki itokee ndipo mamlaka zianze kukimbizana na madhara ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kuzuilika.

Nashauri mamlaka nyingine kote nchini kujifunza kutoka TARURA Dodoma kwa kufanya ukaguzi wa miundombinu katika maeneo yao na kubaini mapema maeneo hatarishi, ili yafanyiwe maboresho kabla maafa hayajatokea.

Ushirikishwaji wa wananchi pia ni muhimu katika maandalizi hayo. Wananchi wanapaswa kupewa nafasi ya kutoa taarifa kuhusu maeneo hatarishi katika makazi yao, yakiwemo mashimo na madimbwi ambayo yanaweza kuwa hatari kwa watoto. Aidha, mifereji ya kupitisha maji inapaswa kujengwa au kurekebishwa ipasavyo ili kuelekeza maji kwenye maeneo salama na kuzuia yasienee katika makazi ya watu.

Kinachotia wasiwasi ni kwamba, katika maeneo mengi bado kuna miundombinu ambayo haijaandaliwa vya kutosha kwa ajili ya kupokea na kuelekeza maji ya mvua. Barabara nyingi hazina mifereji yenye uwezo wa kutosha kupitisha maji, hali inayoweza kusababisha maji kusambaa au kutuama katika eneo moja na hatimaye kuleta madhara kwa wananchi.

Aidha, zipo barabara zilizochongwa hivi karibuni katika baadhi ya maeneo, lakini hazijawekewa changarawe, makalavati au mifereji ya maji.

Katika baadhi ya maeneo, uchongaji wa barabara umeathiri hata mwelekeo wa asili wa maji. Hali hii inaweza kurekebishwa mapema kwa kuweka makalavati na kuchimba mifereji itakayosaidia maji kufuata njia salama bila kuathiri barabara, makazi na shughuli za wananchi.

Kwa upande mwingine, Serikali inapaswa kurahisisha taratibu za utoaji wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya maandalizi hayo, ili fedha ziwafikie TARURA na mamlaka nyingine kwa wakati na kuwawezesha kuanza kazi mapema. Muda uliobaki kuelekea kipindi cha mvua ni mfupi, hivyo ucheleweshaji wa fedha unaweza kuchelewesha pia utekelezaji wa hatua muhimu za kinga.

Tumewaona viongozi mbalimbali, akiwemo Makamu wa Rais, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, wakitoa maelekezo ya kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo. 

Hata hivyo, utekelezaji wa maagizo hayo unapaswa kuonekana hadi ngazi za chini, ambako ndiko wananchi wanakokumbana moja kwa moja na madhara ya miundombinu isiyoandaliwa vizuri.

Kwa hiyo, jambo hili linapaswa kuanzia kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na viongozi wengine katika maeneo yao. 

Wanapaswa kusimamia maandalizi hayo na kuhakikisha TARURA na mamlaka nyingine zinazohusika zinapata fedha na rasilimali zinazohitajika kwa wakati, kwa ajili ya kuboresha miundombinu.

Tusisubiri mvua zianze kunyesha na madhara yatokee ndipo tuanze kutafuta suluhisho. Maandalizi ya mapema ni nafuu zaidi kuliko kukabiliana na madhara baada ya kutokea.

Mwisho, wananchi wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mvua hizo katika nyanja zote hasa katika masuala ya kilimo, kiuchumi, kiusalama na kiafya kwa upande wa magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu. 

Elimu hiyo itawasaidia kuchukua tahadhari mapema, kulinda maisha na mali zao na kushirikiana na mamlaka katika kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
 

Post a Comment

0 Comments