Mradi wa ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi ya Abiria mjini Shinyanga, umefikia hatua inayoleta matumaini kwa wananchi, baada ya majengo mengi yanayotakiwa katika kituo hicho kukamilika katika hatua za awali, ikiwa ni takribani asilimia 48 ya hatua zote za ujenzi.
Kukamilika kwa kituo hicho cha kisasa kinachojengwa katika
eneo la Katunda Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, kunatarajiwa
kuchochea uchumi kwa wananchi wa Shinyanga, kuweka mazingira bora, salama na ya
kisasa kwa ajili ya huduma za usafiri wa mabasi, pamoja kuboresha taswira ya
mji wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mshauri wa Mradi huo Emannuel Kisimba, hatua iliyofikiwa hivi sasa ni ya kuridhisha na kwamba, ujenzi wa Stendi hiyo ambao umeanza kutekelezwa tarehe 25 Oktoba, 2025, unatarajiwa kukamilika tarehe 27, Januari, 2027.
Mradi huo uliopo chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, ambao utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni
5.787 mpaka kukamilika kwake, unatekelezwa na Kampuni ya SIHOTECH ENGINEERING LIMITED, kwa kushirikiana na kampuni ya AMJ GLOBAL MULTI- CONTRACTORS ya jijini Dodoma.
Mhandisi Kisimba amekieleza kituo hicho kuwa kitakuwa na miundombinu mbalimbali ambayo ni pamoja Jengo la utawala litakalokuwa na eneo la mapumziko ya abiria, eneo la maegesho ya mabasi lenye uwezo wa kuhimili mabasi 25 kwa wakati mmoja na eneo la kulaza mabasi 11 kwa wakati mmoja.
Amesema kituo hicho pia kitakuwa na eneo la maegesho ya
magari, bajaji na pikipiki kwa ajili ya abiria, choo cha umma na Kituo cha
polisi.
Pia, kitakuwa na kibanda cha walinzi, sehemu ya kukusanyia
taka, Tenki la maji na kijumba cha Jenereta kwa ajili ya umeme wa dharura.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mhandisi Boaz Kayira, amesema wanatarajia utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho utakamilika kwa wakati, ambapo ameendelea kutoa msisitizo kwa Mkandarasi kuongeza kasi zaidi.
0 Comments