Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth
Magomi, amekutana na wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi mkoani humo na
kuwataka kuzingatia sheria, kanuni na masharti yanayosimamia uendeshaji wa
kampuni hizo.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Bwalo la Polisi mjini Shinyanga, SACP Magomi aliwataka kuhakikisha kampuni zao zinazingatia matakwa yote ya kisheria, ikiwemo kujisajili katika mfumo wa usimamizi na uratibu wa kampuni binafsi za ulinzi (Private Security Companies Portal).
Kamanda Magomi alionya kuwa, Kampuni zitakazokiuka masharti ya sheria zinaweza kupoteza uhalali wa kufanya shughuli za ulinzi, ikiwemo kusitishwa kwa vibali walivyopewa.
Aidha, SACP Magomi aliwasisitiza wamiliki hao kuhakikisha Askari wa kampuni zao wanakaguliwa wakati wanapoingia na kutoka kazini, ili kudhibiti ukiukwaji wa maadili ya kazi na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utu, usafi na nidhamu.



0 Comments