Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Dkt. Francis Mlacha, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kuzingatia misingi ya upendo, utu, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ili kupunguza malalamiko na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Mhe. Mlacha ametoa wito huo leo, Oktoba 27, 2026, alipokutana na kuzungumza na watumishi wa Manispaa ya Kahama kwa ajili ya kujitambulisha, katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri, akisisitiza umuhimu wa watumishi kutambua kuwa dhamira kuu ya utumishi wa umma ni kuwahudumia wananchi.
Amesema watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa upendo na utu, huku wakihakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati bila kupotezewa muda, akieleza kuwa misingi hiyo itasaidia kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kupunguza malalamiko yanayoweza kutatuliwa katika ngazi za chini.“Siwezi kuumia hata siku moja kwa kuhudumia watu. Ninaamini tunapaswa kutoa huduma kwa upendo na utu,” amesisitiza.
Aidha, amewataka watumishi kuacha tabia ya kujiona kuwa wao ni bora kuliko wengine, kunyanyasa au kudhalilisha wananchi na watumishi wenzao, akibainisha kuwa kila mtu anastahili kuheshimiwa na kushirikishwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Amesema pale mtumishi anapobainika kukiuka taratibu, hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa, badala ya kutumia nafasi za uongozi kuwaonea wengine.
Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa watumishi kuwa na nidhamu ya muda (punctuality), kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa tayari kwenda kutatua changamoto za wananchi, badala ya kujifungia ofisini na kusubiri wananchi wafike kutafuta huduma.
Ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kuacha kutoa sababu zisizo za msingi za kutowajibika, akiwakumbusha kuwa matokeo ya utendaji wao yanatokana na maamuzi na matendo wanayoyafanya kila siku.
Kuhusu usimamizi wa miradi ya maendeleo, Mhe. Dkt. Mlacha amewataka watumishi kufuatilia kwa karibu shughuli na miradi iliyoanzishwa ili kuhakikisha inatekelezwa na kukamilika kwa ufanisi, huku wakitenganisha majukumu ya kiutumishi na masuala ya kisiasa.
Ameahidi kushirikiana na watumishi hao katika kusimamia shughuli za maendeleo ya Manispaa ya Kahama, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utazingatia utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa taratibu na maslahi ya wananchi.
Vilevile, amewataka watumishi kutunza mazingira ya kazi, kuwa wawazi na kujenga utamaduni wa mshikamano, akieleza kuwa uwajibikaji wenye matokeo chanya unahitaji umoja na ushirikiano miongoni mwa watumishi katika ngazi zote.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Ndg. Masudi Kibetu, alimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya na kumshukuru kwa kuanza kuitangaza Manispaa ya Kahama katika kipindi kifupi tangu alipofika, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kusukuma mbele maendeleo ya eneo hilo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Bi. Glory Absalum, alimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya na kupongeza mchango wa watumishi wa Manispaa, akieleza kuwa wamekuwa wakishirikiana vizuri katika kutekeleza majukumu yao kwa ajili ya maendeleo ya Manispaa.

0 Comments