FAHAMU MAJUKUMU YA OFISI YA HUDUMA ZA UANGALIZI KWA WALIOHUKUMIWA KIFUNGO CHA NJE KWA MAKOSA YA JINAI

Afisa Huduma za uangalizi Wilaya ya Shinyanga Godfrey Andrew

Ofisi ya huduma za uangalizi ambayo iko chini ya Wizara ya mambo ya ndani ya nchi, pamoja na mambo mengine, imepewa mamlaka na sheria ya kuhudhuria na kusikiliza mashauri ya jinai mahakamani, kusimamia wafungwa wa vifungo vya nje na kusimamia utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

Kwa mujibu wa Afisa uangalizi (Afisa Probesheni) wilaya ya Shinyanga Godfrey Andrew, hukumu ya kifungo cha nje kwa waliopatikana na hatia kwa makosa ya jinai, inatolewa kukidhi matakwa ya sheria ya huduma kwa jamii namba 6 ya mwaka 2002 sura 291 na sheria ya kifungo cha nje kwa wahalifu sura 247, ambazo zote kwa pamoja zimelenga kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani ikiwemo gharama za kuwatunza.

Andrew amevitaja vigezo vya mtu aliyepatikana na hatia kwa makosa ya jinai kufungwa kifungo cha nje kuwa ni pamoja na kosa alilolifanya kutozidi kifungo cha miaka minne, awe raia wa Tanzania, awe mkosaji wa mara ya kwanza kwa makosa ya jinai, na awe na makazi maalum na wadhamini ambao ni ndugu zake wa karibu.

Amesema kifungo cha nje pia kinaweza kutolewa kutokana na pendekezo la maafisa wa magereza, ambao sheria inawaruhusu kumwombea mfungwa kumalizia adhabu yake kwa kifungo cha nje, ambaye hukumu yake haizidi miaka minne na ameonyesha nidhamu wakati akiwa gerezani .

Bw. ndrew amebainisha kwamba, kifungo cha nje wakati mwingine kinaweza kutolewa kwa watu kutoka makundi maalum kama vile, wanafunzi, wajawazito, wazee, wenye changamoto ya akili na wenye changamoto za kiuchumi pale inapotokea wamekutwa na hatia mahakamani kwa makosa ya jinai ambayo vifungo vyake havizidi miaka minne.

Amesema kwa upande wa kundi hilo, wao hawapewi adhabu mbadala ya kufanya shughuli za kijamii kama ilivyo kwa wengine na badala yake kwa wanafunzi wanapewa nafasi ya kuendelea na masomo huku wengine wakihudhuria mafunzo ya kurekebisha tabia kupitia maafisa kutoka Ofisi ya uangalizi yanayotolewa mara mbili kwa mwezi.

Aidha kwa wale wenye changamoto ya akili hupewa rufaa kwenda kwenye taasisi ambazo zitawasimamia na kuhakikisha usalama wao.

Akifafanua zaidi ameleeza kuwa, kabla ya Mahakama kutoa uamuzi wa mwisho, Hakimu hupima uzito wa kosa na madhara yaliyotokea kutokana na kosa hilo na baadaye huishirikisha Ofisi ya uangalizi kwa ajili ya kufanya uchunguzi kwenye jamii,  ili kubaini endapo mshitakiwa anakidhi vigezo vilivyowekwa na kama hawezi kusababisha madhara au yeye mwenyewe kupata madhara pale atakapofugwa kifungo cha nje.

Amesema uamuzi wa mwisho wa Mahakama huzingatia taarifa ya maandishi iliyowasilishwa kutoka Ofisi ya Uangalizi, na baada ya hukumu kutolewa, Mfungwa hukabidhiwa kwa maafisa wa uangalizi ambao humpeleka kwenye Ofisi za umma kwa ajili ya kufanya shughuli za kijamii bila malipo, chini ya usimamizi wao mpaka pale muda wa kifungo chake utakapomalizika.

Aidha, kabla ya hukumu kutolewa, mhusika hutakiwa kukubali masharti ambayo ni pamoja na kuhudhuria kila siku na kwa muda unaotakiwa mahali alipongwa kwa ajili ya kufanya shughuli za kijamii, kuwa tayari kutekeleza maelekezo ya msimazi aliyepewa na kuwa mwaminifu na mwenye tabia njema katika kipindi chote cha kifungo.

Masharti mengine ni kuripoti kwa Afisa uangalizi kila anapohitajika, kupokea maelekezo anayopewa, kujiepusha na makundi hatarishi ambayo yanaweza kumfanya atendo makosa mengine, na hatakiwi kuhama wala kuondoka kwenye makazi anayoishi kwa kipindi chote cha kifungo bila idhini ya Ofisi ya uangalizi.  

Bw. Andrew amewaomba wananchi kutohofia kutembelea Ofisi za ungalizi zilizopo karibu yao ili kupata elimu na kupewa ushauri wa kitaalam, kwa kuwa Ofisi hizo zimewekwa na Serikali kwa ajili ya umma wote wa watanzania. Ofisi hizo ziko katika mikoa na wilaya zote nchini.

Katika kipindi cha kuanzia Julai 1, mwaka 2022, hadi  Oktoba ,25 mwaka 2026, jumla ya watu 322, waliopatikana na hatia kwa makosa mbalimbali ya jinai mkoani Shinyanga, wamehukumiwa kifungo cha nje.

Hukumu hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu.

Post a Comment

0 Comments