![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita |
NA SIMEO MAKOBA-SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, kesho Alhamisi, Oktoba 22, 2026, anatarajiwa kuzindua rasmi kimkoa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote, inayolenga kuwawezesha Watanzania wote kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Kwa mujibu
wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Honoratha Rutatinisibwa, uzinduzi huo
utafanyika katika Uwanja wa Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga, kuanzia saa 3:00
asubuhi, na utahudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya pamoja na
wananchi.
Amesema awamu hiyo itahusisha usajili wa Watanzania wote bila kujali makundi yao, tofauti na awamu ya kwanza ambayo ililenga zaidi wananchi kutoka kaya zisizo na uwezo ambao ni wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Dkt. Rutatinisibwa amefafanua kwamba, baada ya uzinduzi huo, wananchi wataweza kujisajili kwenye Bima ya Afya kwa Wote kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mawakala wengine walioidhinishwa na Serikali.
Kuhusu gharama, Dkt. Rutatinisibwa amesema, bima hiyo itagharimu shilingi 150,000 kwa mwaka, kwa kaya yenye watu wasiozidi sita, wakiwemo mwanachama mchangiaji, mwenza wake na watoto wanne.
Amebainisha kuwa, wanachama watakaosajiliwa kupitia mpango huo watanufaika na huduma za afya za msingi zipatazo 372, kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka Hospitali za rufaa.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi huo na kutumia fursa hiyo kuanza kujisajili, ili waweze kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu.
Bima ya Afya kwa Wote ni mpango wa Serikali unaolenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila kuzuiwa na changamoto za kiuchumi.
Mpango huo ambao utazinduliwa kwenye mikoa nchi nzima hapo kesho, unatarajiwa kupunguza mzigo wa gharama za matibabu ambao wananchi hukabiliana nao wanapolazimika kulipia huduma hizo moja kwa moja.

0 Comments