CHEREHANI ALILIA BARABARA YA LAMI KWA WAZIRI MKUU

 

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani, ameiomba Serikali kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kahama–Ushetu yenye urefu wa kilometa 54, akieleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika Jimbo la Ushetu, Cherehani amesema Wilaya ya Kahama ina majimbo matatu ambayo ni Ushetu, Msalala na Kahama Mjini, lakini majimbo ya Msalala na Kahama Mjini tayari yana miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa barabara za lami, lakini Jimbo lake halina mradi wowote mkubwa.

Amesema kutokana na umuhimu wa barabara ya kutoka mjini Kahama kwenda Ushetu, Serikali ianze ujenzi hata kwa awamu, ili wananchi wa Ushetu waonje uzuri wa miundombinu bora ya barabara.

Aidha, Cherehani ameiomba Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Halmashauri ya Ushetu, ili kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya ufundi stadi bila kulazimika kwenda Kahama au Msalala.

Ameeleza kuwa baadhi ya familia hazina uwezo wa kugharamia usafiri na malazi ya watoto wao wanapokwenda kusoma katika maeneo hayo, hivyo uwepo wa chuo hicho ndani ya Halmashauri utasaidia kupanua fursa za elimu na ujuzi kwa vijana, hususan wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.

Akifafanua ombi lake kuhusu miradi ya barabara, Cherehani amesema:

“Wilaya ya Kahama ina majimbo matatu. Wabunge wenzangu wa majimbo ya Msalala na Kahama Mjini wana miradi mikubwa ya kimkakati ya barabara na ipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.

Najua umejionea barabara yetu wakati unakuja hapa. Tunaomba na sisi tupate mradi wa kimkakati utakaotupa kujivunia,” amesema Cherehani.

Kufuatia maombi hayo ya Mbunge, Waziri Mkuu Nchemba amemwelekeza Meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Shinyanga kuharakisha usanifu wa barabara hiyo, ili iweze kuingizwa kwenye mpango wa Bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

 

Post a Comment

0 Comments