![]() |
| Askofu Mteule wa kwanza wa Jimbo jipya la Nzega, Mheshimiwa Joseph Mashaka Triphon (C.S.Sp) |
Mpaka
kuteuliwa kwake, Padre Mashaka alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa
Bikira Maria, Kanisa kuu Jimbo Katoliki la Bagamoyo.
Askofu
mteule Joseph Mashaka Triphon, alizaliwa tarehe 15 Januari 1962 nchini Tanzania,
ambapo baada ya malezi na majiundo yake ya Kipadre na Kitawa, tarehe 1 Oktoba
1994 aliweka Nadhiri za daima na tarehe 27 Mei 1995 akapewa Daraja Takatifu ya
Upadre.
Kati ya
Mwaka 1995 hadi mwaka 2003, aliteuliwa kuwa Mratibu wa shughuli za kichungaji kwa
wanafunzi wa Shirika, ambapo kati ya Mwaka 1996 hadi 1998 alitumwa na Shirika
kujiendeleza katika masomo katika Chuo
Kikuu cha Strasburg, kilichoko nchini Ufaransa.
Kati ya
Mwaka 2003 hadi mwaka 2010, alichaguliwa kuwa Mchumi wa Shirika Kanda ya Afrika
ya Mashariki.
Kati ya Mwaka 2010 hadi mwaka 2012, alijiendeleza katika masuala ya
ushauri Chuo Kikuu cha Lambeth, kilichoko nchini Uingereza ambapo baada ya kurejea nchini Tanzania, alihudumia kama Paroko msaidizi Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi,
Kipawa, Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2012 hadi
Mwaka 2016.
Mwaka 2012
hadi mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shule ya Libermann ambapo Mwaka
2016 hadi mwaka 2021 akateuliwa kuwa Paroko wa Kipawa na Dekano wa Dekania ya
Segerea.
Kati ya
Mwaka 2021 hadi 2025, alitumwa kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa
Amani, Jimbo Katoliki Kigoma, huko Kasumo ambako pia aliteuliwa pia kuwa Dekano
wa Watawa.
Kuanzia
Mwaka 2025 akateuliwa kuwa Paroko wa Kanisa kuu la Moyo Safi wa Bikira Maria
Jimbo Katoliki Bagamoyo, mpaka alipoteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Nzega leo.
Jimbo jipya
la Nzega, linatokana na kugawanywa kwa Jimbo kuu la Tabora, na linakuwa Jimbo la
38 nchini Tanzania.
Makao makuu ya Jimbo jipya la Nzega yatakuwa mjini Nzega na kuunganisha
Wilaya ya Nzega na Igunga, Mkoa wa Tabora.
Kanisa kuu
la Jimbo jipya la Nzega litakuwa ni Parokia ya Mtakatifu Bernadetta.
Jimbo jipya
la Nzega lina eneo ya Km za mraba 14, 237, lenye
wakazi 1, 263, 147 na kati ya hao, waamini wa Kanisa Katoliki ni 139, 304.
Jimbo hilo
kwa sasa litakuwa na jumla ya Parokia 13 na Parokia teule 2, Mapadre wa jimbo
25 na Mapadre watawa 8, Shemasi 1, Mtawa wa kiume ni 1 na watawa wa kike ni 66.
Litakuwa na
taasisi mbalimbali za kanisa ambazo ni pamoja na Hospitali 5 na Taasisi za
Elimu ni 11.

0 Comments