DIWANI SAWA ATAMBULISHA MRADI WA UJENZI WA DARAJA LA MINZI KWA WANANCHI, AWATAKA KUULINDA DHIDI HUJUMA

Diwani wa Kata ya Ndembezi Mh.Pendo Sawa ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga akizungumza na wananchi

Diwani wa Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, Mheshimiwa Pendo Sawa, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kusimamia rasilimali zitakazotumika katika mradi wa ujenzi wa Daraja la Minzi linalojengwa katika Kata hiyo, unaotarajiwa kuanza rasmi kesho Jumatatu, tarehe 9, Novemba, 2026.

Akizungumza katika mkutano maalum wa kutambulisha mradi huo kwa wananchi uliofanyika kwenye eneo la mradi, Mheshimiwa Sawa amesema wananchi wana wajibu wa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa usalama na bila hujuma za aina yoyote, ili ukamilike kwa wakati uliopangwa na kuinufaisha jamii nzima.

Amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa uongozi na mamlaka  nyingine zinazohusika pindi wanapobaini viashiria vya hujuma, ikiwemo wizi wa vifaa na mali nyingine za mradi, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza kuomba ajira zitakazotolewa katika mradi huo, akisisitiza kuwa, mkandarasi anapaswa kutoa kipaumbele kwa wakazi wa eneo hilo katika nafasi za kazi hususan zisizohitaji utaalamu maalum.

Mheshimiwa Sawa ameahidi kushirikiana na wananchi kuhakikisha kuwa kipaumbele hicho kinazingatiwa, katika utekelezaji wa mradi huo.

Mkutano huo umehudhuriwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Ndembezi hususan wakazi wa mitaa ya Mbuyuni, Dome na Mabambasi ambao ni wanufaika wa moja kwa moja wa mradi huo, wakiwemo viongozi wa mitaa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, wameahidi kushirikiana na diwani wao kuhakikisha vitendo vya hujuma dhidi mradi huo vinadhibitiwa.

Wamesema kukamilika kwa daraja hilo kutatoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya mawasiliano iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu na kuwawezesha kutekeleza shughuli zao za maendeleo kwa urahisi, hasa wanapohitaji kwenda au kutoka upande mwingine wa eneo hilo.

Mradi huo wa ujenzi wa daraja ambalo linaunganisha mitaa ya Mbuyuni na Dome, Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, unatekelezwa na Kampuni ya PAMVIC Co. Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 112 na unatarajiwa kukamilika Mei 7, 2027.




Post a Comment

0 Comments