WAZIRI MKUU DKT. NCHEMBA AAGIZA WAGONJWA WA DHARURA NA WAJAWAZITO KUTOCHELESHEWA HUDUMA

Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka watoa huduma katika sekta ya afya kuhakikisha wajawazito na wagonjwa wa dharura wanapatiwa huduma bila kucheleweshwa, pale tu wanapofika kwenye Zahanati, vituo vya afya na Hospitali kwa ajili ya kupata huduma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Novemba 8, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kishapu kupitia mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye uwanja ya SHIRECU wilayani humo.

Amesema kuwalazimisha wagonjwa wa namna hiyo kufuata taratibu za kiutawala ni uzembe unaweza kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika.

Ametolea mfano wa mama mjamzito anayefikishwa hospitalini akiwa na uchungu wa kujifungua, lakini badala ya kuhudumiwa anaulizwa maswali yasiyo ya msingi ambayo ni pamoja na beseni la kujifungulia, hali inayoweza kuchelewesha huduma na kusababisha madhara kwa mama na mtoto ikiwemo kifo. 

 Amesema Serikali haitakubali mazoea ya namna hiyo katika taasisi za umma. 

 Aidha, Mheshimiwa Mwigulu amezitaka hospitali kutowachangisha wagonjwa fedha za mafuta ya gari la wagonjwa wa dharura kwani ni huduma inayopaswa kutolewa na Serikali, akisisitiza kuwa, kipaumbele cha Serikali ni kuokoa maisha. 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Nchemba amemwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe.Paschal Patrobas Katambi, kuhakikisha anasimamia suala la Polisi kutowanyang'anya wala kushikilia vyombo vya moto vya wananchi wanaofanya makosa yenye adhabu ya faini na badala yake ufanyike utaratibu wa kulipa faini wanayodaiwa huku wakiendelea na shughuli zao. 

Wakati huohuo, ameitaka Wizara ya Ujenzi kuharakisha usanifu wa barabara ya Kolandoto–Mwangongo, ili iingizwe katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028, huku maandalizi yakizingatia madaraja, njia itakayopita na fidia kwa wananchi watakaoguswa. 

 Waziri mkuu Nchemba yuko mkoani Shinyanga kwa ziara ya siku nne, ambapo Jumatatu tarehe 9, Novemba 2026, atafanya ziara katika Jimbo la Solwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Badaye katika Manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi(Katikati), Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro(wa kwanza kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Dkt. Francis Mlacha(wa kwanza Kushoto)
Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga Mbala Mlolwa
Waziri wa mambo ya Ndani ya nchi na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini Paschal Patrobas Katambai
Waziri wa Ujenzi Masanja Kadogosa
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Shinyanga na Naibu waziri wa Nishati Salome Makamba
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye Picha ya pamoja Wilayani Kishapu
Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Pili Mnyami
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Lucy Mayenga

Post a Comment

0 Comments