MRADI WA UJENZI WA DARAJA LA MINZI KATA YA NDEMBEZI KUANZA RASMI JUMATATU

 

Mradi wa ujenzi wa Daraja la Minzi, linalounganisha mitaa ya Mbuyuni na Dome katika Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, unatarajiwa kuanza rasmi Jumatatu, Novemba 9, 2026, huku mkandarasi akiwa tayari ameanza maandalizi ya awali ya ujenzi huo.

Katika maandalizi hayo, mkandarasi ameanza kubomoa daraja la zamani ili kupisha ujenzi wa daraja jipya, linalotarajiwa kuondoa changamoto ya hofu ya kusombwa na maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaotumia njia hiyo, hususan wakati wa mvua, ambapo daraja la awali lilishindwa kuhimili ongezeko la maji.


Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Salvatory Yambi, amesema ujenzi wa daraja hilo unatekelezwa na Kampuni ya PAMVIC Co. Ltd, kwa gharama ya shilingi milioni 112 na unatarajiwa kukamilika Mei 7, 2027.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ndembezi, Pendo Sawa, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Sawa ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, amesema kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa suluhisho la changamoto ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi, kutokana na daraja dogo lililokuwepo kushindwa kuhimili ongezeko la maji wakati wa mvua, hali iliyokuwa ikisababisha hofu na usumbufu kwa watumiaji wa njia hiyo.

Nao baadhi ya wananchi wanaotumia njia hiyo wakiwemo wakazi wa maeneo jirani wamepongeza hatua hiyo ya Serikali ya kulijenga upya daraja hilo, ambalo limekuwa kikwazo wakati wa kutekeleza shughuli zao hasa wakati wa masika.


Post a Comment

0 Comments