SERIKALI KUANZA KUWALIPA FIDIA WAFUGAJI WALIOSHINDA KESI MAHAKAMANI

 Na Samwel Mwanga-Meatu Simiyu.
SERIKALI imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 3.8 kwa ajili ya kuwalipa fidia wafugaji ambao mifugo yao ilitaifishwa na baadaye kushinda kesi mahakamani.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema wizara ya fedha imeanza mchakato wa malipo hayo, ambapo kila mfugaji atalipwa kulingana na thamani ya mifugo yake iliyotaifishwa.
Akizungumza Novemba 7, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mwandoya, wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, amesema uamuzi huo umetokana na serikali kubaini madhara yaliyowakumba wafugaji kutokana na utekelezaji wa sheria iliyokuwa ikiruhusu utaifishaji wa mifugo.
Amesema serikali iliamua kuifuta sheria hiyo baada ya kubaini kuwa ilikuwa chanzo cha malalamiko makubwa kwa wafugaji, hususan wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Meatu ni miongoni mwa wilaya zinazopakana na Pori la Akiba la Maswa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambako baadhi ya wafugaji waliathirika na zoezi hilo kwa kupoteza mifugo yao.
"Wizara ya Fedha tayari imeanza zoezi hilo kwa ajili ya kuwalipa wafugaji hao, hivyo utalipwa fidia ya fedha kulingana na thamani ya ng'ombe zako," amesema.

Akizungumzia uamuzi huo, Juma Malando mfugaji mkazi wa Mwandoya, amesema malipo ya fidia ni muhimu kwa wafugaji waliopoteza mifugo yao, lakini akaomba serikali kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wahusika kwa wakati.

"Tumekuwa tukisubiri haki yetu kwa muda mrefu baada ya kupoteza mifugo yetu. Uamuzi wa Serikali kutenga fedha za fidia umetupa matumaini, lakini tunaomba malipo yafanyike kwa uwazi ili kila mfugaji aliyestahili aweze kurejesha shughuli zake za ufugaji," amesema.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mussa Mbuga, aliwasilisha changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, zikiwemo ukosefu wa maji safi na salama pamoja na gharama kubwa  za kulimiwa na matrekta yaliyotolewa na Bodi ya Pamba.

Amesema wakulima wanatozwa Sh 55,000 kwa ekari moja, hali aliyosema ni mzigo kwao, hivyo kuiomba serikali iingilie kati ili gharama hizo zipunguzwe hadi Sh45,000.

Charles Shema ni mkulima wa pamba kutoka Kisesa, amesema gharama hizo zinawaongezea wakulima mzigo wa uzalishaji, hasa wale wenye mashamba makubwa.

"Gharama ya Sh55,000 kwa ekari moja ni kubwa kwa wakulima wengi. Tukilimia ekari nyingi tunatumia fedha nyingi kabla hata ya kuanza kupata mavuno. Tunaomba gharama zipunguzwe hadi Sh45,000 ili wakulima wengi waweze kumudu huduma hiyo na kuongeza uzalishaji," amesema.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments