SHINYANGA KESHO KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAUME

 

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga anayeratibu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanaume, Omary Jumanne

Mkoa wa Shinyanga kesho, Novemba 19, utaungana na maeneo mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanaume, kwa kufanya mijadala mbalimbali kuhusu nafasi ya wanaume katika familia na jamii.

Akizungumza na SHINYANGA ONE MEDIA, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga anayeratibu maadhimisho hayo, Omary Jumanne, amesema mijadala  itajikita katika mada mbalimbali, zikiwemo nafasi ya mwanaume katika malezi ya watoto, mchango wake katika maendeleo ya jamii pamoja na changamoto zinazoathiri utekelezaji wa majukumu yake katika familia na jamii.

Jumanne ameeleza kuwa washiriki wa maadhimisho hayo wanatarajiwa kutoka katika makundi mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa Umoja wa Wanaume Mkoa wa Shinyanga, taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na makundi mengine ya kijamii.

Amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo yataanza saa 2:00 asubuhi.

Siku ya Kimataifa ya Wanaume huadhimishwa Novemba 19 kila mwaka. Ilianzishwa rasmi mwaka 1999 nchini Trinidad na Tobago kwa lengo la kutambua mchango chanya wa wanaume katika familia na jamii, kuhamasisha afya na ustawi wao, pamoja na kujenga uelewa kuhusu usawa wa kijinsia na malezi bora.

 

Post a Comment

0 Comments